Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Mei 24, 2024 Local time: 23:05

Uganda: Polisi waendelea kutumia nguvu dhidi ya upinzani,vifo vyaripotiwa, majibizano yaongezeka kwenye mitandao


Mgombea wa urais Uganda Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine, akiwa katika kampeni Nov. 30, 2020.
Mgombea wa urais Uganda Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine, akiwa katika kampeni Nov. 30, 2020.

Mlinzi wa Bobi Wine auawa katika mazingira tatanishi

Mlinzi wa mgombea wa urais Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine, amefariki duniani katika mazingira tatanishi Jumapili.

Ripoti za vyombo vya habari Uganda vinakariri mashahidi wakisema kwamba Francis Kalibala, aligongwa na gari la jeshi la Uganda UPDF wakati msafara wa Bobi Wine ulikuwa unarudi Kampala kutoka Masaka katika kampeni.

Katika taarifa kupitia mitandao ya kijamii Bobi Wine amesema “nasikitika kutangaza kifo cha mmoja wa walinzi wangu Francis Kalibala aliyegongwa na gari la jeshi namba H4DF 2382 ambalo liliziba njia karibu na Busega na kutuzuia kupita.” Ameandika Bobi Wine na kuongeza kusema“Francis amefariki mda mfupi baada ya kufika katika hospitali ya Rubaga.”

Lakini msemaji wa jeshi la Uganda Brig. Flavia Byekwaso amesema katika taarifa kwa vyombo vya habari kwamba Francis alianguka kutoka kwa gari lililokuwa linaendeshwa kwa mwendo wa kasi.

“Francis hakugongwa na gari la jeshi la UPDF. Alianguka kutoka kwa gari namba UBF 850Z .” amesema Byekwaso katika ujumbe wa twitter.

Waandishi wa habari wajeruhiwa vibaya

Kabla ya tukio hilo, waandishi kadhaa wa habari walishambuliwa na polisi na kujeruhiwa vibaya.

Waandishi hao walikuwa wanafuatilia tukio ambalo polisi walimzuia Bobi Wine kufanya kampeni na kuzua makabiliano kati ya polisi na wafuasi wa Bobi wine katika mji wa Masakaa.

Waandishi walipigwa na kujeruhiwa na mabomu ya kutoa machozi.

Wamelazwa hospitalini mjini Masaka.

Miongoni mwao ni mpiga picha wa televisheni ya Bobi Wine ya Ghetto TV, Ashraf Kasirye, mwandishi wa shirika la habari la Nation Media Group – NTV Ali Mivule.

“Gesi ya kutoa machozi ilitumika kutawanya wafuasi wa Bobi Wine na kwa bahati mbaya waandishi wa habari walijeruhiwa,” amesema msemaji wa polisi Fred Enanga.

Tume ya uchaguzi yapiga marufuku kampeni

Tume ya uchaguzi imepiga marufuku kampeni katika wilaya na miji kadhaa ikisema kwamba wilaya hizo zina idadi kubwa ya maambukizi ya virusi vya Corona na huenda kampeni zinaeneza virusi hivyo hatari.

Wilaya hizo ni Pamoja na Mbarara, Kabarole, Luweero, Kasese, Masaka, Wakiso, Jinja, Kalungu, Kazo, Kampala na Tororo.

Wanasiasa wa upinzani hata hivyo wamesema hatua hiyo ni ya kisiasa kwa sababu sehemu ambapo kampeni zimepigwa marufuku ni ngome za kisiasa hasa za mgombea wa urais Bobi Wine.

Rais Yoweri Museveni ambaye anagombea urais kwa mhula wa sita, amemaliza kufanya kampeni katika baadhi ya sehemu hizo na ndizo ambazo zimesalia kwa Bobi Wine.

Tume ya uchaguzi hata hivyo, imesema kwamba rais Museveni anaweza kuendelea kuzindua miradi ya serikali katika sehemu ambazo kampeni zimepigwa marufuku.

“Hatua ya tume ya uchaguzi imeniathiri sana. Wilaya ya Wakiso ina wapiga kura milioni 1.5 Kampala ina wapiga kura milioni moja, Jinja na Masaka zina maelfu ya wapiga kura. Najiuliza, ni wapi nitatoa kura iwapo sitafanya kampeni?” amesema Generali Henry Tukukunde, mgombea wa urais.

Wagombea wa viti mbalimbali wametakiwa kutumia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kufanya kampeni.

Idadi ya wapiga kura katika wilaya ambapo tume ya uchaguzi imepiga marufuku kampeni ya moja kwa moja.

Kampala (wapiga kura 1,281.308), Wakiso (1,160,551), Kasese (372,102), Mukono (354,047) Jinja (274,772) Tororo (264,222) Luweero (256,454)

Muhoozi Kainerugaba: Wakoloni wanaounga mkono upinzani watashindwa

Mwana wa kiume wa Rais Yoweri Museveni, ambaye ni kamanda wa kikosi maalum cha jeshi kinachomlinda Rais Museveni Lt. Gen. Muhoozi Kainerugaba ameonya wale aliwataja kama “wakoloni wanaounga mkono upinzani nchini Uganda” akisema kwamba watashindwa vibaya sana katika uchaguzi mkuu wa Jnauari 14.

Muhoozi ameandika kwenye twitter, baada ya wakili wa Bobi Wine Robert Amsterdam kuandika ujumbe wa twitter, akitaka jumuiya ya kimataifa kuingilia kati na kuwaajibisha maafisa katika serikali ya Uganda baada ya polisi kuwajeruhi waandishi wa habari Jumapili asubuhi.

Muhoozi amejibu ujumbe huo kwamba “wakoloni wanajaribu kubadilisha rangi yao lakini kila mzalendo anawajua!”

Muhoozi ambaye vile vile ni mshauri wa babake kuhusu shughuli maalum amemalizia ujumbe wake kwa kutumia maneno ya kwanza ya wimbo wa taifa wa Afrika kusini “Nkosi Sikelei iAfrica” maana yake, “Mungu ibariki Afrika!”. Muhoozi amemalizia ujumbe huo kwa kusema “Waafrika watashinda wale wote ambao kila mara wanataka kuwatawala.”

Maafisa wa Uganda akiwemo balozi wajibizana na mkuu wa tume ya kutetea haki za kibinadamu

Maafisa wa ngazi ya juu katika serikali ya Uganda wamemshambulia mkuu wa shirika la kufuatilia haki za kibinadamu -Human Rights Watch, Ken Roth wakimshutumu kwa kuingilia katika siasa za nchi hiyo.

Miongoni mwa maafisa waliomshambulia Roth ni balozi wa Uganda katika Umoja wa Mataifa Adonia Ayebare, baada ya kukosoa hatua ya tume ya uchaguzi kupiga marufuku kampeni za moja kwa moja katika wilaya kadhaa ambazo wachambuzi wa siasa Uganda wanasema Bobi Wine ana umaarufu mkubwa.

Tume ya uchaguzi imepiga marufuku kampeni kwa msingi kwamba hatua hiyo inalenga kuzuia maambukizi ya virusi vya Corona.

“Tafadhali achana kabisa na siasa za Uganda pamoja na mikakati yetu ya kupambana na virusi vya Corona. Hatuna haja na ukosoaji wako,” ameandika Balozi Ayebaye akiongeza kwamba Ken Roth ameshindwa kabisa kutekeleza kazi yake katika shirika la kufuatilia haki za kibinadamu – Human Rights Watch na kuangusha shirika hilo kwa jumla.

“Shirika la HRW limekuwa kundi la wanaharakati wa kisiasa kwa lengo la kuvuruga siasa za Afrika,” ameongezea kuandika balozi Ayebare.

Mashambulizi hayo ya twitter dhidi ya Ken Roth pia yamemhusisha msimamizi wa habari wa Rais Yoweri Museveni Don Wanyama, aliyeandika “swala la ni nani maarufu wapi, litaamuliwa na wapiga kura wa Uganda Januari 14 na wala sio mawakala wa ukoloni wanakaa katika nchi za magahribi. Heshimu uhuru wetu.”

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC.

XS
SM
MD
LG