Mashekhe 18 wamekamatwa wiki iliyopita na polisi nchini Uganda kufuatia wimbi la mauaji ya kushangaza ya mashekhe nchini humo.
Kwa mujibu wa duru za habari jijini Kampala kuna makundi mawili yanayo gongana katika misikiti miwili mikubwa, mmoja uko eneo la Nakasero na mwingine mjini Kampala.
Akiongea na VOA, Sheikh mmoja kwa sharti kutotajwa jina amesema kwamba Baraza Kuu la Umoja wa Waislamu Uganda limegawanyika katika makundi matatu. Lakini makundi mawili ambayo yaliamua kujitoa katika baraza hilo hayatambuliwi na serikali.
“Kundi ambalo linatambuliwa na serikali ni lile ambalo ofisi zake ziko Old Kampala, mengine ambayo yako Kibuli na Nakasero hayatambuliwi,” alifafanua.
Pande hizo zimehasimiana na zimeendelea kushutumiana na inasemekana zimeshindwa kufikiasuluhu. Mpaka sasa jumla ya mashekhe waliotiwa kizuizini ni 45.
Lakini wachambuzi wa mambo ya dini wanasema tatizo lililopo linafungamana na ushindani wa makundi haya mawili ambayo sasa imechukua sura mpya baada ya baadhi ya viongozi wa dini kuuwawa.
“Kinachotokea hivi sasa kila wakati sheikh anapouliwa kutoka upande mmoja, pande nyingine zinanyoosha vidole kulaumu kundi jingine na hivyo polisi huenda na kuwakamata watu hao,” alielezea kwa undani.
Mtu mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema hadi hivi sasa idadi ya masheikh waliouwawa imefikia 17, na kati yao wanne ni masheikh maarufu nchini Uganda.
Lakini habari tulizopokea kutoka katika duru za kiislamu nchini Uganda zinasema imekuwa vigumu kwa Baraza Kuu la Umoja wa Waislam Uganda kusuluhisha mgogoro huu kutokana na kugawanyika kwa chombo hicho katika makundi matatu.
“Baraza limegawanyika na kumekuwa na pande ambazo zinavutana,” alisema mtoaji habari kwa sharti jina lake lisitajwe.
Lakini katika juhudi za kutafuta suluhu kati ya makundi haya bunge la Uganda lilijaribu kuingilia kati suala hili mara tu pale mauaji yalipoanza na kuiomba polisi kuchukua hatua mara moja.
Moja ya kero za wabunge waliokuwa wanajadili mada hii bungeni ilikuwa kitendo cha polisi kuvamia misikiti na kuifunga mashariki mwa Uganda, kitu ambacho kilikuwa kinaingilia uhuru wa kuabudu, alisema mmoja wa wabunge hao.
Lakini kuna pia taarifa kwamba kukamatwa kwa mashekhe kunatokana na kifo cha meja Sulaiman Kigundu aliyeuwawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana. Dereva wake pia aliuwawa katika tukio hilo.
Chanzo cha habari hii kinaeleza kuwa mashekhe hawa wanashukiwa kuwa wamehusika na kifo hicho.
“Tunaelezwa na jeshi la polisi kwamba wameshikiliwa ili kusaidia katika upelelezi wa vifo hivyo,” alisema moja wa waumini mjini Kampala.
Kigundu alikuwa mmoja wa wapiganaji wa chama cha Allied Demokratic Forces ambaye serikali ya Uganda ilimpa msamaha ili ajisalimishe.
ADF ni kundi la waasi kinachoipinga serikali ya Uganda na kinatambulika kama kundi la kigaidi.