Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Aprili 15, 2024 Local time: 00:13

Uganda kupeleka wafanyakazi wa afya nje ya nchi


Wafanyakazi wa huduma ya afya nchini Uganda
Wafanyakazi wa huduma ya afya nchini Uganda

Wizara ya mambo ya nje nchini Uganda imeandaa mpango ambao utapeleka wafanyakazi wa huduma za afya takribani 300 wenye ujuzi wa juu katika nchi za Trinidan na Tobago. Wakosoaji wanasema huduma za afya Uganda tayari ni mbaya sana na kwamba Zaidi ya waganda milioni moja watapoteza huduma za afya kwa sababu ya hatua hiyo.

Kwa miaka kadhaa nchi ya Uganda imekuwa ikitaabika kutokana na upungufu wa wafanyakazi wa huduma za afya. Mafunzo ya wastani pamoja na mishahara duni na ukosefu wa vifaa vimechangia wafanyakazi wengi wa idara hiyo kutafuta kazi mahala kwingine au kuhamia nje ya nchi.

Serikali ya nchi hiyo hivi sasa inaanda mpango wa orodha ya wafanyakazi wa huduma za afya 283 wenye kiwango cha juu kupelekwa Trinidad na Tobago kufanya kazi huko. Maafisa wa program wanasema miongoni mwa idadi hiyo kuna wakunga 185, wafanyakazi 20 wa kitengo cha maabara kwa picha kati ya 28 waliopo nchini humo na mfanyakazi mmoja kati ya watatu wenye utaalamu wa upasuaji wa mwili.

Wizara ya mambo ya nje nchini humo ina matumaini kwamba program hiyo italeta manufaa nyumbani kwamba pesa zitatumwa nyumbani na wafanyakazi hao na kulipiwa kodi hivyo kuweza kuchangia katika kuongeza fedha kwa sekta ya huduma ya afya.

Muuguzi wa afya akichukua damu kutoka kwa mgonjwa
Muuguzi wa afya akichukua damu kutoka kwa mgonjwa

Uganda ina kiasi cha daktari mmoja kwa kila wagonjwa 25,000 na muuguzi mmoja kwa kila wagonjwa 11,000. Idadi hizo imepelekea kuongezeka viwango vya vifo vinavyoweza kuzuilika na kuongezeka idadi ya vifo vya uzazi ambapo wanawake 17 wanafariki kila siku kutokana na matatizo ya kujifungua.

Janet Obuni ni rais wa chama cha wauguzi na wakunga nchini Uganda alisema program za kufanya kazi nje ya nchi zinavutia kwa sababu ni jambo la kawaida kwa wauguzi kufanya kazi bila kulipwa hadi miezi sita. Lakini anakiri kuwa kuwapeleka wafanyakazi wa huduma ya afya nje ya nchi kutawaweka wagonjwa wengi hatarini nchini humo.

Hata hivyo Fred Opolot, msemaji wa wizara ya mambo ya nje Uganda alisema kwamba serikali inauangalia utaratibu huu kwa karibu.

Alisema wizara ya mambo ya nje inafanya kazi kwa karibu sana na wizara ya afya na wizara ya kazi na jinsia nchini Uganda. Pia wamehakikisha kwamba vyovyote wanavyofanya hawataiweka nchi katika hali ambayo itasababisha hatari kwa maisha ya waganda. Hizi ni juhudi mbadala zilizopangwa na kuna matumaini kwamba kwa kuwapeleka wafanyakazi wa afya huko Trinidad na Tobago haitahatarisha mfumo wa afya nchini Uganda.

XS
SM
MD
LG