Mji mkuu wa Uganda, Kampala wenye takriban wakazi milioni 2 ni miongoni mwa miji yenye hewa chafu ulimwenguni, huku viwango vikiwa mara 7 zaidi ya vile vinavyoruhusiwa na shirika la afya duniani WHO, kulingana na ripoti ya ubora wa hewa iliyotolewa mwaka uliopita.
Mhandisi ambaye pia anaongoza utafiti kwenye chuo kikuu cha Makerere jijini Kampala Bain Omugisa amesema kwamba hatua hiyo imechochewa na ongezeko la vifo kutokana na uchafuzi wa hewa ulimwenguni. Uchafuzi wa hewa unalaumiwa kusababisha asilimia 15 ya vifo kulingana na ripoti ya mwaka 2017 ya kundi la kimazingira la Alliance on Health and Pollution. GAHP.
Takriban watu 28,000 hufa kila mwaka nchini Uganda kutokana na uchafuzi wa hali ya hewa kulingana na kundi la GAHP. Kifaa kipya cha kudhibiti ubora wa hewa nchini humo kimefadhiliwa kwa kiasi na kampuni ya Google, wakati kikitumia sensa ya aina fulani, ikiwa na gharama ya dola 150 za kimerekani kwa ajili ya kukagua ubora wa hewa kwenye jiji la Kampala.