Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Mei 24, 2024 Local time: 22:30

Uganda yaakaribisha kampeni dhidi ya LRA


Joseph Kony, kiongozi wa kundi la uasi nchini Uganda la Lord's Resistance Army-LRA
Joseph Kony, kiongozi wa kundi la uasi nchini Uganda la Lord's Resistance Army-LRA

Serikali ya Uganda imeidhinisha kampeni za kwenye mtandao dhidi ya LRA lakini yaonya kampeni yeyote lazima iendane na ukweli kuhusu kundi hilo

Uganda inasema inakaribisha kampeni za kwenye mtandao dhidi ya kundi la uasi la Lord’s Resistance Army-LRA lakini inaonya dhidi ya kutia chumvi kitisho kwa LRA.

Katika taarifa yake iliyochapishwa kwenye gazeti linalomilikiwa na serikali ya Uganda la New Vision, serikali ya nchi hiyo iliidhinisha kampeni ili kuongeza ufahamu wa kulijua kundi la LRA na hali ya waathirika wa kundi hilo la uasi huo.

Lakini ilisema kampeni yeyote iendane na ukweli kuhusu kundi hilo la LRA.
Wiki iliyopita kundi moja la wanaharakati la Invisible Children lilitumia mtandao wa Twitter kuleta mwamko wa filamu kuhusu kundi la LRA na kiongozi wake, Joseph Kony, ambaye anatafutwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu-ICC. Filamu hiyo imeangaliwa zaidi ya mara milioni 70 kwenye mtandao wa You Tube.

Hata hivyo watengenezaji wa filamu hiyo wamekosolewa kwa kupotosha ukweli halisi juu ya matukio.

Serikali Jumatatu ilieleza kwamba kundi la LRA halifanyi harakati zake tena nchini Uganda na ilisema waasi wamesambaratika na hawana nguvu ambapo kundi sasa limebaki na wapiganaji chini ya 300.

Kundi hilo linaendelea kushambulia vijiji kadhaa nchini Congo na Jamhuri ya Afrika ya kati lakini Uganda inasema kitisho kinacholetwa na LRA katika nchi hizo kinaonekana kimepungua sana.

Kundi la LRA lilipigana na majeshi ya serikali huko kaskazini mwa Uganda kwa zaidi ya miaka 15 kabla ya kuondoka nchini humo mwaka 2006. Kundi hilo linafahamika kwa kuwateka nyara watoto na kuwatumia kama wanajeshi na watumwa wa ngono na linashutumiwa kwa mauaji na kuwakata viungo maelfu ya watu.

Kony na viongozi wengine watatu wa LRA wanatafutwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu-ICC kwa mashtaka ya uhalifu wa vita na uhalifu dhidi ya binadamu.

Mwaka jana, Rais wa Marekani Barack Obama alipeleka washauri 100 wa masuala ya kijeshi huko Afrika ya kati ili kuyasaidia majeshi ya Uganda kuwasaka wapiganaji waliobaki wa LRA.

XS
SM
MD
LG