Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Juni 23, 2024 Local time: 07:13

Mzozo wa uvuvi wazuka kati ya Kenya na Uganda.


Wavuvi katika ziwa Victoria.
Wavuvi katika ziwa Victoria.

Jumuiya ya Afrika Mashariki ingali kwenye mkondo wa kuwaleta wananchi wake pamoja na kujenga shirikisho lenye nguvu na endelevu katika uchumi na siasa. Lakini hili bado likishughulikiwa, uhasama unaonekana kuhusu ziwa victoria hususan kati ya Kenya na Uganda, huenda ukakwamiza juhudi hizo.

Mara kwa mara wavuvi wa Kenya hasa kwenye ufukwe wa ziwa hilo eneo la Marenga na eneo bunge la Budalang’i katika kaunti ya Busia wamekuwa wakilalamika kuhangaishwa na maafisa wa usalama wa Uganda katika ziwa hilo.

Wiki hii, wavuvi wapatao wanane waliokuwa wakivua samaki katika kisiwa cha Bumeru karibu na kisiwa cha Sigulu kilichopo Kenya walikamatwa na maafisa hao kwa tuhuma za kuvua samaki pasi kuwa na vyombo vilivyo rasmi na hivyo basi kupelekwa katika mahakama moja katika wilaya ya Namayingo nchini Uganda.

Msemaji wa Mahakama Kuu ya Uganda Solomon Muyita alithibitisha suala hilo.

Stephen Masaa mwenyekiti wa usimamizi wa shughuli za uvuvi katika ufukwe wa Omena Beach eneo la Marenga aliweza kufika katika mahakama hiyo ya Namayingo nchini Uganda Jumanne. Bwana Masaa anaeleza kuwa kisa hiki si cha kwanza kutokea kwani wavuvi wa ufukwe wa ziwa hilo eneo la Marenga wamekuwa wakikamatwa na maafisa wa usalama wa Uganda kila mara wanapojikuta katika sehemu ya Uganda.

Baadhi ya wavuvi katika ufukwe wa ukanda huu wanaeleza kukasirika kwao na kujikokota kwa serikali ya Kenya kuwahakikishia usalama mara tu wanapojitosa katika shughuli za uvuvi katika ziwa hilo.

Raia wa Kenya wanaoishi kando ya Ziwa Victoria wanachuma riziki yao kutokana na shughuli za uvuvi na hivyo basi kuwepo kwa mgogoro wa aina hii, bila shaka huathiri kwa kiasi kikubwa mustakabali wao.

Wachuuzi wa samaki eneo la Marenga Port Victoria vile vile wanaiomba serikali kuingilia kati na kukomesha hatua za maafisa wa usalama wa Uganda kuingia katika ufukwe wao na kuwakamata wavuvi wa eneo hilo.

XS
SM
MD
LG