Marekani inasema uchaguzi wa rais ulofanyika hivi karibuni huko Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo ulikuwa na kasoro nyingi.
Katika taarifa iliyotolewa Jumatano msemaji wa wizara ya mambo ya nje Victoria Nuland amesema tathmini ya Marekani imetokana na ripoti za timu za wafuatiliaji zilizopelekwa na Marekani na nchi nyenginezo pamoja na makundi huru ya wafuatiliaji uchaguzi.
Nuland alisema haikufahamika, hata hivyo, kama kasoro hizo na ukosefu wa uwazi unegeweza kubadili matokeo ya uchaguzi huo.
Alitoa wito kwa wakuu wa Congo kufanya uchunguzi wa haraka wa kiufundi katika utaratibu wa uchaguzi ambao anasema utasaidia kuamua ikiwa kasoro zinatokana na uzembe katika maandalizi au ni kutokana na wizi moja kwa moja. Nuland anasema Marekani iko tayari kutoa msaada wake wa kiufundi kwa ajili ya uchunguzi huo.
Kwa upande mwengine, waziri wa habari wa Congo Lambert Mende amesema wanadiplomasia wanakubali kwamba rais Joseph Kabila alishinda uchaguzi ulokua na utata. Walitangaza maoni yao Jumatano usiku.
Mende anasema walieleza wasi wasi wao kuhusiana na jinsi Tume Huru ya Uchaguzi CENi iliyosimamia uchaguzi wa rais na wa bunge wa Novemba 28. Matamshi ya waziri yalitolewa baada maafisa wa serikali kukutana na wanadiplomasia kutoka nchi za nje kutafakari juu ya uchaguzi wamwezi uliyopita