Makubaliano hayo yanafuatia wiki kadhaa za mazungumzo na Umoja wa Ulaya ambao uliahidi msaada mkubwa kwa Tunisia wa euro bilioni 1 kusaidia kufufua uchumi wa Tunisia unaodorora, kuokoa fedha za serikali na kukabiliana na mzozo wa wahamiaji.
Fedha nyingi kati ya hizo zitatumiwa kufanya mageuzi ya kiuchumi.
“Makubaliano hayo yana mikataba ya kusitisha biashara ya usafirishaji haramu wa watu na wasafirishaji wa binadamu, kuimarisha usalama wa mipaka na kuboresha uandikishaji wa watu wanaoingia na kutoka. Hatua zote muhimu za kuimarisha juhudi za kukomesha uhamiaji usio wa kawaida,” waziri mkuu wa Uholanzi Mark Rutte alisema kwenye Twitter.
Mkuu wa Tume ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen alisema jumuiya hiyo itatoa euro milioni 100 kwa Tunisia kusaidia kupambana na uhamiaji haramu.
Makubaliano hayo yanaimarisha uthabiti wa uchumi, biashara na uwekezaji, matumizi ya nishati ya kijani na uhamiaji halali.
Maelfu ya wahamiaji haramu kutoka nchi za Afrika waliingia kwa wingi katika mji wa Sfax katika miezi ya karibuni wakitaka kuelekea Ulaya kwa kutumia boti za wasafirishaji haramu wa binadamu, na kusababisha mzozo wa wahamiaji ambao haujawahi kushuhudiwa nchini Tunisia.
Forum