Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Machi 29, 2024 Local time: 02:31

Tume ya uchaguzi Kenya yasikiliza maoni ya Wakenya Marekani


Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Kenya Issack Hassan (katikati) akikutana na wajumbe wa tume yake.
Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Kenya Issack Hassan (katikati) akikutana na wajumbe wa tume yake.

Kufuatana na katiba mpya tume ya uchaguzi ya Kenya imeanza ziara ya nchi za nje ili kutayarisha namna ya kupanga uchaguzi kufanyika nje ya nchi.

Kenya inapoadhimisha miaka 48 ya uhuru iliyonyakua kutoka Uingereza Disemba 12 1963, Wakenya wanatafakari na kujadili namna ya kutekeleza katiba mpya inayoleta mabadiliko makubwa ya kisiasa, kijamii, na haki za kiraia.

Mojawapo ya mabadiliko makubwa ni kuwaruhusu Wakenya wanaoishi katika nchi za nje kuweza kupiga kura katika uchaguzi unaofanyika nchini humo. Na mtihani mkubwa ni uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka 2012.

Kutokana na hali hiyo, maafisa wa tume ya uchaguzi na mipaka IEBC wakiongozwa na mwenyekiti wa tume Ahmed Issack Hassan, unatembelea miji mikubwa ya Marekani na kusikiliza maoni ya wananchi wa nchi hiyo, ili kutafakari namna ya kupanga zowezi hilo nje ya nchi kwa mara ya kwanza.

Kwa ushirikiano na ubalozi wa Kenya mjini Washington, chama kipya cha wa Wakenya wanaoishi jimbo la New England, kaskazini mashariki ya Marekani kilianda sherehe za uhuru mjini Boston na kuwapatia Wakenya fursa ya kukutana na wajumbe wa IEBC, kujadili masuala yanayohusiana na uchaguzi.

Owere Omondi, afisa wa chama hicho ameiambia Sauti ya Amerika kwamba kuna masuala muhimu yanayobidi kutanzuliwa kabla ya zowezi hilo kuweza kufanyika. Anasema "kuna suala la uwandikishaji wapiga kura, jee ni hati gani wanabidi kuonesha kuthibitisha uraia wao? Na ikiwa wakenya walochukua uraia wa Marekani wataruhusiwa kushiriki".

Katiba mpya ya Kenya inaruhusu raia kuwa na uraia wa nchi ya kigeni bila ya kupoteza uraia wake wa Kenya, lakini hadi hivi sasa bunge halijapitisha sheria zinazohitajika ili kutekeleza sheria ya katiba.

XS
SM
MD
LG