Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Februari 09, 2023 Local time: 03:12

Tume ya mawasiliano Uganda inataka Google kufunga vituo kadhaa vya You tube


Mgombea wa urais nchini Uganda Robert Kyagulanyi akiwa mahakamani

Tume inayosimamia mawasiliano nchini Uganda (UCC) imeandika barua kwa kampuni ya Marekani ya Google, ikiitaka kampuni hiyo ifunge stesheni kadhaa za televisheni zinazopeperusha matangazo yake kupitia You tube.

Miongoni mwa stesheni hizo ni Ghetto TV, inayomilikiwa na chama cha National Unity Platform (NUP), cha mgombea wa urais Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine.

UCC inataka karibu stesheni 13 zinazopeperusha matangazo yake moja kwa moja kupitia You tube, kufungwa kwa msingi kwamba zimekiuka sheria na maadili ya habari nchini Uganda.

Barua ya UCC kwa Google inasema kwamba “tume ya mawasiliano ya Uganda imepokea malalamiko kadhaa kutoka kwa maafisa wa serikali akiwemo waziri wa mambo ya ndani, mwenyekiti wa usalama wa taifa, polisi na jeshi la nchi hiyo kuhusu habari zinazopeperushwa na vituo hivyo vinavyotumia You tube na kwamba vinapeperusha habari ambazo zinavunja sheria ya mawasiliano ya Uganda, ya mwaka 2013 na sheria inayosimamia habari ya mwaka 2019, ibara ya 8 sehemu ya 2.”

Televisheni ambazo zimetajwa kwenye barua ya UCC ni pamoja na TMO Online, Lumbuye Fred, Trending Channel Ug, Uganda Yaffe, Uganda News Updates, Ghetto TV, Busesa Media Updates, Uganda Empya, Map Mediya TV, KK TV, Ekyooto TV, Namungo Media, JB Muwonge na Bobi Wine 2021.

Barua hiyo inadai kwamba televisheni hizo kwenye mtandao wa You tube, zilitumika kueneza machafuko ya hivi karibuni nchini Uganda yaliyopelekea vifo vya watu kadhaa na uharibifu wa mali.

Inaendelea kusema kwamba zinatumika “kueneza habari za uongo, na maoni potofu kwa nia ya kupotosha jamii, zikiwa na lengo la kusababisha ghasia kwa misingi ya kikabila na kisiasa.”

Barua hiyo inaongezea kwamba habari na maoni yanayopeperushwa na stesheni hizo “yana upendeleo, yanaonyesha miili ya watu waliokufa, waliojeruhiwa vibaya, ajali mbaya na zinaweza kusababisha wasiwasi mkubwa katika jamii.”

UCC inasema kwamba televisheni hizo za mtandao wa You tube, hazina leseni ya kupeperusha habari nchini Uganda.

Kulingana na ibara ya 27 ya sheria ya maudhui nchini Uganda, hakuna mtu anaruhusiwa kupeperusha habari bila ya kuwa na leseni ya tume ya mawasiliano ya nchi hiyo na anayefanya hivyo anaweza kuhukumiwa mwaka mmoja gerezani, kulipa faini au kulipa faini na kifungo cha mwaka mmoja gerezani.

“Kwa hivyo, kwa kuzingatia sheria ya mawasiliano ya mwaka 2013 namba 5(1) (b), (j), (x), 6 na 45, Tume inataka Google kufunga kabisa stesheni hizo,” inasema barua ya UCC kwa kampuni ya Google.

Mapema mwaka huu, tume ya mawasiliano nchini Uganda UCC, iliamuru watu wote wanaoandika maudhui kwenye mitandao ya kijamii kusajili kurasa zao la sivyo wachukuliwe hatua za kisheria.

Agizo hilo hata hivyo linaripotiwa kutotiliwa maanani.

Hatua hiyo inajiri wakati tume ya uchaguzi nchini humo inataka wagombea wote kufanya kampeni kwa njia ya internet kutumia mitandao ya You tube, Facebook, Twitter na kadhalika pamoja na radio, televisheni, kutokana na janga la virusi vya Corona.

Stesheni ambazo UCC inataka zifungwe zinaonyesa sana kampeni za wanasiasa wa upinzani.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG