Trump alitoa tangazo hilo la kushangaza Jumanne jioni baada ya kukutana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu huko White House.
Wakati maelfu ya wakazi wa Gaza wakirudi katika nyumba zao zilizobomolewa kufuatia makubaliano ya sitisho la mapigano la Januari 19 kati ya Israel na Hamas, Rais Trump siku ya Jumanne alitoa tangazo la kushangaza.
Donald Trump, Rais wa Marekani: "Marekani itauchukua Ukanda wa Gaza na tutaifanyia kazi."
Matamshi hayo ya Trump yanavuka yale aliyosema mwezi uliyopita kwamba atawahamisha wakazi wa Gaza hadi nchi jirani za Jordan na Misri.
Anasema anataka kujenga eneo hilo kuwa alichokiita “mandhari ya Kitalii ya Riviera katika Mashariki ya Kati.
Donald Trump, Rais wa Marekani kila mtu niliyezungumza naye amelipenda wazo la Marekani kumiliki eneo hilo, kulijenga na kubuni maelfu ya nafasi za ajira, na kulibadili kuwa la kuvutia ambalo hakuna atakayelitambua.
Hakuna mtu anayetaka kuliangalia kwasababu wanachoona ni vifo na uharibifu na vifusi.
Trump alitoa tangazo hilo baada ya kumkaribisha Waziri mkuu wa Israel Benjamina Netanyahu huko White House.
Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel: "Nimesema hili hapo kabla. Ninasema tena Wewe ndiye rafiki mkubwa wa Israel kuwahi kuwepo hapa White House."
Trump hakufafanua jinsi anavyopanga kuchukua udhibiti wa Gaza eneo ambalo limeharibiwa na miezi 15 ya vita. Hakufuta uwezekano wa kupeleka wanajeshi wa Marekani. Haiko bayana kuikalia Gaza kutaingiliana vipi na lengo la Trump mwenyewe la kupanua mkataba wa Abraham kuihusisha Riyadh. Mkataba ambao aliousimamia ambao ulianzisha uhusiano kati ya Israel na nchi za Kiarabu mwaka 2020.
Saudi Arabia imesema itakubali kuitambua Israel ikiwa tu vita vya Gaza vinamalizika na Wapalestina wanapata taifa lao.
Mirette Mabrouk, Taasisi ya Mashariki ya Kati anasema: "Kuwahamisha Wapalestina kwenda mataifa jirani sio mwanzo mzuri, kwa hivyo ninadhani itakuwa na athari kubwa, zaidi ya hapo hatujui, mambo yatakavyo kuwa na Rais Trump, itatubidi tusubiri tuone."
Tangazo la trump kuhusu Gaza ni ishara yake ya karibuni ya dhamira ya upanuzi, kufuatia taarifa zake za awali za kuichukua Greenland kutoka Denmark, kuuchukua Mfereji wa Panama na kuiunganisha Canada na Marekani.
Kabla ya mkutano wake na Netanyahu, Trump aliamuru kurudisha tena kampeni yake ya kuishinikiza Iran ili kuizuia kupata silaha ya nyuklia. Vile vile alisitisha misaada kwa shirika la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya wakimbizi wa Palestina na kuiondoa Marekani kutoka baraza la haki za Bindamu la Umoja wa Mataifa ambayo anasema inachukia Wayahudi.
Forum