White House imetangaza Jumatatu kwamba Rais wa Marekani Donald Trump anaunga mkono juhudi za serikali kuu za kuimarisha uchunguzi wa wateja wanaotaka kununua bunduki hatua ambayo amefikia baada ya mauwaji ya wiki iliyopita yaliyosababisha vifo vya watu 17 kwenye shule ya sekondari ya Marjory Stoneman Douglas iliyoko Parkland katika jimbo la Florida.
Msemaji wa White House, Sarah Huckabee Sanders alisema Rais Trump alizungumza wiki iliyopita na seneta wa jimbo la Texas, m-Republican John Cornyn kuhusu muswada wake unaoshirikisha vyama vyote akiwemo seneta wa Connectcut, m-Democrat Chris Murphy mwanaharakati wa siku nyingi anayepinga bunduki, kwamba kunahitajika kuboresha uchunguzi kwa wanunuaji bunduki.
Mswada huo bado unajadiliwa. Polisi wa Florida walisema Nikolas Cruz mwenye umri wa miaka 19 aliwauwa wanafunzi 14 na watu wazima watatu huko Parkland, Florida kwenye shule ya sekondari ambayo alisimamishwa masomo tangu mwaka jana na aliweza kununua bunduki aina ya AR-15 baada ya kufanyiwa uchunguzi usiokuwa na kanuni kali na kupita kirahisi.
Cruz alisimama mahakamani Jumatatu wakati mawakili wakizungumzia masuala ya utaratibu wa kesi ya mauaji dhidi yake.