Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Mei 23, 2024 Local time: 03:05

Timu nzima ya kampeni na walinzi wa Bobi Wine wazuiliwa na polisi


Mgombea urais nchini Uganda Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine, baada ya kukamatwa alipowasili kisiwani Kalangala katikati mwa Uganda, Dec. 30, 2020.
Mgombea urais nchini Uganda Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine, baada ya kukamatwa alipowasili kisiwani Kalangala katikati mwa Uganda, Dec. 30, 2020.

Mgombea urais nchini Uganda Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, amesema kwamba ataendelea kufanya kampeni, siku moja baada ya polisi na wanajeshi kumkamata na kumsafirisha kwa ndege ya jeshi kutoka kisiwa cha Kalangala hadi Kampala na kumpeleka hadi nyumbani kwake chini ya ulinzi mkali.

Watu kadhaa wakiwemo walinzi na wasimamizi wa kampeni ya Bobi Wine walikamatwa na bado wanazuiliwa na polisi katika kituo cha polisi cha mjini Masaka.

Wine amesema kwamba lengo la maafisa wa polisi ni kumzuia kufanya kampeni, kwa kuwakamata maafisa wake wote wanaosimamia kampeni.

Amesema ataendelea na kampeni katika wilaya za Bukomansimbi na Mpigi, kulingana na mpangilio wa tume ya uchaguzi.

Amesema kwamba ameamua kuendelea na kampeni bila walinzi wake “kwa sababu hivyo ndivyo wanavyotaka maafisa wa usalama nchini Uganda.”

“Hatua ya kuwakamata walinzi na wasimamizi wa kampeni yangu haitatuzuia kuendelea na kampeni kwa sababu sio kwa ajili yangu wala timu yangu ya kampeni. Ni kwa ajili ya Uganda.” Amesema Wine.

‘Mimi na timu yangu tulikubaliana kwamba tutaendelea na kampeni hata kama watamuua mmoja wetu au kutukamata. Nitaendelea kufanya kampeni hata kama nitakuwa nimesalia pekee yangu. Nina uhakika kwamba mahali wenzangu wanazuliwa, wana furaha kwamba naendelea kufanya kampeni.” Ameendelea kusema Wine.

Zaidi ya wasimamizi 90 wa kampeni za Wine walikamatwa Jumatano adhuhuri walipowasili katika kisiwa cha Kalangala kufanya kampeni.

Waandishi wa habari waliokuwa wakifuatilia kampeni ya Bobi Wine nao walikamatwa lakini wakaachiliwa baadaye.

Baadhi wameripoti kupokonywa vifaa vyao vya kazi na simu kuharibiwa.

Waandishi wa habari walikuwa wamefunguliwa mashtaka ya kuripoti kampeni ya Bobi Wine.

Bobi Wine amesema kwamba “lengo kubwa la polisi ni kupunguza kasi yake ya kampeni.”

Hata hivyo, polisi wamesema kwamba waliokamatwa “walinaswa kwenye video za CCTV wakidunga misumari matairi ya magari ya polisi na kutoa hewa, wamechochea ghasia, kuzuia polisi kufanya kazi yao na kushindwa kufuata masharti ya maafisa wa afya katika kudhibithi maambukizi ya virusi vya corona nchini Uganda.”

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG