Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Rex Tillerson ameakhirisha matukio aliyokuwa ayafanye Jumamosi huko Kenya ili kujipumzisha baada ya ratiba iliyojaa shughuli nyingi kulingana na taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Marekani.
Msemaji wa wizara hiyo Steve Goldstein ambaye ameongozana na bwana Tillerson kwenye ziara hii ya bara la Afrika alisema kwamba waziri huyo hajisikii vizuri kiafya baada ya siku kadhaa za kufanya kazi kwa masaa mengi juu ya masuala muhimu yanayoendelea nyumbani Marekani kama vile suala la Korea kaskazini na kwamba ameakhirisha matukio yake hapo nchini Kenya kwa leo Jumamosi.
Tillerson ataendelea na ratiba yake Kenya siku ya Jumapili. Wakati huo huo waziri huyo wa mambo ya nje wa Marekani, Rex Tillerson alisema Ijumaa kwamba maridhiano ya kisiasa kati ya Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga ni hatua kubwa yenye kuleta matumaini, huku akiongeza kwamba Marekani inaunga mkono ushirikishwaji wa kisiasa na demokrasia.
Alipokuwa kwenye mkutano wa waandishi wa habari na kiongozi mwenzake waziri wa mambo ya nje wa Kenya, Monica Juma, bwana Tillerson alisisitiza umuhimu wa uhuru wa vyombo vya habari katika demokrasia na alisema serikali haitakiwi kuvinyamazisha vyombo vya habari.