Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Machi 29, 2024 Local time: 10:51

Tanzania yawapa nasaha wanajeshi wanaolinda amani


Gambo, Central African Republic
Gambo, Central African Republic

Wanajeshi wa Tanzania wanaolinda amani wametakiwa wasikatishwe tamaa na matukio ya mashambulizi wakati wanapokuwa katika ulinzi wa amani kwa kuwa wanatimiza wajibu wao.

Nasaha hiyo ilitolewa wakati wa kuuaga mwili wa mwanajeshi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Nsevilwe Nzowa, aliyeuawa kwenye mashambulizi katika nchi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, gazeti la Nipashe limeripoti.

WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga la Taifa Dkt Hussein Mwinyi, alitoa nasaha hizo akiongeza kuwa msiba huo ni wa kitaifa na tukio hilo limewasikitisha, hivyo wasikate tamaa kwa kuwa wanatekeleza wajibu wao wa kazi.

“Msikate tamaa sisi kama nchi tunafanyakazi nzuri sio tu kwa Jamhuri ya Afrika ya kati tunathaminiwa na Umoja wa Mataifa, hili tukio lilikuwa ni la kushtukiza haliwezi kuzuilika,” alisema Dkt Mwinyi.

Aidha, alisema serikali itachukua kila aina ya hatua kuhakikisha matukio kama hayo yanadhibitiwa ili vijana waweze kufanyakazi zao vizuri.

"Alisema kwa sasa imeundwa tume ambayo itakwenda kuchunguza matukio hayo na baada ya kupatiwa ripoti watachukua tahadhari ili watu wasiendelee kupoteza maisha,” alisema Dkt Mwinyi.

Shughuli za kuaga mwili huo zilifanyika katika hospitali ya jeshi Lugalo na kuhudhuriwa na makatibu wa wizara ya ulinzi, Dk. Florence Turuka na Katibu Mkuu ofisi ya Rais.

Wengine ni wakuu wa majeshi wastaafu Jenerali Robert Mboma na George Waitara na Mnadhimu Luteni Jenerali Yakub Mohamed ambaye alimwakilisha Mkuu wa Majeshi.

Juni 3, mwaka huu kikundi cha wanajeshi maofisa na askari 90 wakiwa ni sehemu ya kikosi cha kulinda amani kilichopo Jamhuri ya Afrika ya Kati (TANZBATT-1 CAR), kikiwa kwenye jukumu la uwajibikaji kilishambuliwa kwa kushtukizwa na kundi la waasi la Siriri.

Katika mashambulio hayo askari mmoja alipoteza maisha na 18 walijeruhiwa kati yao watano hawakuwa katika hali nzuri.

Baadhi ya askari waliojeruhiwa wapo hospitalini wakiendelea na matibabu.

Shughuli za ulinzi wa amani katika nchi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa Tanzania zilianza hivi karibuni hicho kikiwa kikundi cha kwanza.

XS
SM
MD
LG