Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Novemba 28, 2023 Local time: 22:41

Tanzania yapambana na rushwa katika uchaguzi


Wagombea kadha Tanzania wamekamatwa au kuhojiwa kutokana na tuhuma za rushwa katika ngazi za awali za uchaguzi.

Taasisi ya kupambana na kuzuia rushwa nchini Tanzania, Takukuru, inasema iko katika kampeni kabambe ya kuwakamata wagombea uongozi wanaojihusisha na vitendo vya utoaji wa rushwa ili kuwashawishi wapiga kura.

Akizungumza na Sauti ya Amerika-VOA, Mkurugenzi wa Takukuru Edward Hosea amesema juhudi zinafanyika nchini nzima na tayari maofisa kadhaa wamekamatwa na kuhojiwa na Takukuru dhidi ya vitendo vya rushwa wakati huu wa uchaguzi.

Hosea amefafanua sheria ya gharama za uchaguzi ya mwaka 2010 ambayo ilianza kutumika mwezi wa nne mwaka huu, inayokemea na kukataza mambo ambayo hayaruhusiwi kufanyika wakati wa uchaguzi, uteuzi au kura za maoni ambayo ni pamoja na marufuku kwa wagombea kutembea usiku na kuzungumza na wapiga kura ama wasimamizi wengine wa maeneo wanayogombea pamoja na kutoa zawadi.

Amesema katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu, Takukuru inahakikisha sheria hizo zinazingatiwa nchi nzima na wale watakaokiuka watakamatwa na kuchukuliwa hatua bila kuangalia sura, nafasi ya mtu wala jinsia.

Mkurugenzi huyo wa Takukuru amekiri kuwa kuna mali zilizokamatwa zinazohusika na rushwa, na vilevile kuna wagombea wa ubunge kama mkuu wa wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma Betty Machangu ambaye alikamatwa wiki hii na Takukuru kwa kuwashawishi wapiga kura wamchague kuwa mbunge wa viti maalumu kupitia chama cha CCM mkoa wa Kilimanjaro. Vile vile Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto Margaret Sitta ambaye pia ni mke wa spika wa bunge la Tanzania Samuel Sitta naye ni miongoni mwa waliohojiwa na Takukuru akiwa mkoani Tabora kwa tuhuma za kugawa rushwa ndani ya chama chake .

Zinazohusiana

XS
SM
MD
LG