Akitangaza hatua hiyo, Waziri mkuu Kassim Majaliwa alisema kuwa uamuzi huo ungeanza kutekelezwa kutoka tarehe 17.
Alisema wizara ya elimu itafanya marekebisho ya ratiba kwa wanafunzi wanaotarajiwa kufanya mitihani yao kuanzia tarehe 4 mwezi Mei.
Hali kadhalika nchi hiyo ilisitisha michezo yote inayowaleta pamoja wachezaji na mashabiki wengi au makundi ya watu.
“Serikali imesitisha michezo yote inayokusanya makundi ya watu ikiwamo Ligi Kuu ya Tanzania Bara (VPL), Ligi Daraja la Kwanza (FDL), Ligi Daraja la Pili (SDL) na aina nyngine. Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo iziandikie taasisi zake,” alisema.
Akisisitiza kuwa Tanzania imejiandaa vyema kukabiliana na mlipuko wa COVID 19, Majaliwa aidha alisema mikusanyiko yote ya watu wengi yakiwemo matamasha ya muziki, mikutano ya hadhara mbalimbali imepigwa marufuku kwa sasa.
“Watanzania wenye safari zisizo za lazima kwenye nchi zenye maambukizi makubwa, wanashauriwa wasitishe safari hizo,” alisema Majaliwa.
Majaliwa pia alitoa wito kwa Watanzania kuzingatia ushauri unaotolewa na Serikali na kupuuza "taarifa za uzushi' zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.
“Watanzania tuache mzaha wa kutumia mitandao ya kijamii kufanya upotoshaji wa tahadhari katika jambo hili,” alionya.
Hadi tulipokuwa tukitayarisha ripoti hii, Tanzania ilikuwa imeripoti kisa kimoja cha maambukizi ya Corona.