Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 19, 2024 Local time: 23:54

Mkuu wa Majeshi aeleza hatua zinazochukuliwa baada ya Lissu, Mritaba kupigwa risasi


Jenerali Venance Salvatory Mabeyo
Jenerali Venance Salvatory Mabeyo

MKUU wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo, amezungumzia matukio ya uhalifu wa kupiga watu na risasi yanayoendelea nchini Tanzania, akisema vyombo vya ulinzi vipo kazini na hivi karibuni hali itakuwa shwari.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam Jumatano Jenerali Mabeyo alionyesha kushangazwa na matukio ya sasa kuonyesha kushtua watu wengi, tofauti ya yaliyotokea Kibiti mkoani Pwani, yaliyoua zaidi ya watu 35.

“Kwa nini matukio yaliyotokea Kibiti hayaleti mshtuko mkubwa wakati watu walioathirika Kibiti ni wengi zaidi kuliko matukio ya sasa, mimi sitaki kuingia huko,” alisema.

Alisema kwa matukio ya sasa ya kupiga watu kwa risasi, uzoefu unaonyesha wanaoyatekeleza ni watu ambao hawajapitia kwenye Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

“Vijana wanaohusika katika uhalifu hawajapitia Jeshi la Kujenga Taifa, kwa hiyo tuna imani kabisa vijana wetu wanaopitia Jeshi la Kujenga Taifa wanakuwa na maadili, wanakuwa na nidhamu, nitaomba ninyi mtusaidie katika wale watakaokuwa wamekamatwa katika kuwahoji, tuone kama watakuwa wamepitia Jeshi la Kujenga Taifa,” alisema Jenerali Mabeyo.

Kauli hii imetolewa na Jeshi baada ya matukio makubwa ya watu kupigwa risasi yaliyotokea nchini hivi karibuni, ni pamoja na lile la Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, aliyepigwa risasi Septemba 7 mjini Dodoma na watu wasiojulikana.

Jingine ni lile la Jenerali mstaafu, Vincent Mritaba, aliyepigwa risasi na watu wanaosadikika kuwa ni majambazi wakati akiingia nyumbani kwake Ununio wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam akitoka benki siku tatu zilizopita.

Lissu kwa sasa yupo Nairobi nchini Kenya akiendelea na matibabu, huku hali yake ikielezwa kubadilika badilika wakati Jenerali Mritaba, anatibiwa katika Hospitali ya Jeshi Lugalo, Dar es Salaam na afya yake inaelezwa kuimarika

Jenerali Mabeyo alisema kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vinashughulika na matukio kadiri yanavyojitokeza na anaamini hali itakuwa shwari.

“Matukio yanayoendelea tunakabiliana nayo, vyombo vya ulinzi na usalama wakati wote vinakabiliana na matukio kadiri yanavyojitokeza, Ninaamini hali itakuwa shwari na sasa vinashughulika.

“Hoja ya msingi tunataka kujiridhisha silaha hizi zinatoka wapi, hawa watu ni wa aina gani. Sasa vyombo mviachie vifanye kazi yake, msitoe majibu haraka, tukio linapotokea lazima uangalie limetokeaje, chanzo ni nini, na ‘motive’ (sababu) ni nini,” alisema Jenerali Mabeyo.

XS
SM
MD
LG