Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Septemba 15, 2024 Local time: 23:12

Tanzania: Watanzania watakiwa kuungana ili kupata katiba mpya


Tanzanian President Samia Suluhu Hassan addresses a press conference after her meeting with U.S. Vice President Kamala Harris in Dar es Salaam, Tanzania, March 30, 2023.
Tanzanian President Samia Suluhu Hassan addresses a press conference after her meeting with U.S. Vice President Kamala Harris in Dar es Salaam, Tanzania, March 30, 2023.

Jukwaa la katiba Tanzania (JUKATA) pamoja na wanasheria wamewataka wananchi, taasisi na asasi za kiraia kuungana pamoja katika kudai katiba mpya.

Wadau hao wameitaka serikali kuahirisha mpango wa kutoa elimu kwa miaka mitatu na baadala yake mchakato wa katiba mpya uende sambamba na utoaji wa elimu.

Wito huo unakuja baada ya kauli ya aliyekuwa waziri wa katiba na sheria Dkt Damas Ndumbaro kuelezea mpango wa serikali wa kutoa elimu ya katiba kwa miaka mitatu ambao umepokelewa kwa maoni tofauti.

Oleshangay Joseph mwanasheria kutoka Arusha anasema utoaji wa elimu kwa miaka mitatu utachelewesha mchakato wa kupata katiba mpya hivyo utaratibu wa kutoa elimu unapaswa kwenda pamoja na mchakato wa kutafuta katiba mpya.

“Huwezi katoa elimu ya katiba bila kuanzisha mchakato wa katiba yaani inapaswa iwe ni hatua inayokwenda sambamba. Mchakato uanze ndiyo elimu itolewe kwenye mchakato unatoa elimu ya nini kwa mapendekezo yapi kwahiyo kwangu mimi kauli ya Ndumbaro ni kauli ambayo haistahili kupewa nafasi,” amesema Oleshangay.

Aidha, Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA) limetoa wito ambao wameitaka serikali kuachana na mpango wa kutoa elimu ya katiba ya mwaka 1977 kwa miaka mitatu na baadala yake wapeleke miswaada ya sheria za mchakato wa katiba bungeni ili kufanyiwa marekebisho.

Mkurugenzi wa jukwaa hilo Bob Wangwe akizungumza na sauti ya Amerika amewataka wadau, asasi za kiraia na wananchi kuongeza kasi katika kudai mabadiliko ya katiba kwani ndiyo njia sahihi ya kupata katiba ndani ya muda mfupi.

“Sisi wananchi kwa pamoja tukisimama na wadau mbalimbali wa asasi za kiraia mimi naamini kabisa tutapata katiba ndani ya muda mfupi na sio kama ambavyo huyu waziri wa katiba na sheria alikuwa anadhani kwamba anaweza akatupa elimu miaka mitatu na kuchelewesha mchakato kiujumla.”ameongezea kusema Wangwe

Hata hivyo Deusi Kibamba ambaye ni Mjumbe wa bodi inayoongoza Jukwaa la Katiba, Tanzania amesema wanaochelewesha mchakato wa katiba ni watu wachache wanaonufaika na mapungufu yaliyopo ndani ya katiba ya sasa na hivyo amemtaka Rais Samia Suhuhu Hassani kuwasikiliza wananchi na kuruhusu mchakato wa katiba uanze.

“Hao wanao neemeka na mapungufu ya katiba ya mwaka 1977 kwa kweli wamekuwa wakifanya kila juhudi kukwamisha katiba mpya isipatikane kwa haraka ili waendelee kufaidika na mapengo ya katiba ya mwaka 1977 sasa naliona hili kwamba mheshimiwa Rais amekuwa katikati ya hayo makundi mawili kundi la kwanza akitamani ajiunge nalo alisikilize ni kundi hili la wananchi,”ameongezea Kibamba

Wananchi wanayo nafasi kubwa katika harakati za kudai katiba mpya kwani katiba ni misingi ya haki ambayo inapaswa ituongoze kama nchi amemalizia kusema Oleshangay.

imetayarishwa na mwandishi wetu Amri Ramadhani, Tanzania.

Forum

XS
SM
MD
LG