Tanzania ni moja ya nchi kadhaa ambazo huenda zikakumbwa na masharti maalum kwa raia wake kupewa visa kuja Marekani, kwa mujibu wa rasimu ambayo imeandaliwa na utawala wa Trump kuhusu hatua mpay za uhamiaji.
Rais Donald Trump huenda wiki ijayo akapitisha marufuku ya kusafiri ambayo itazikumba nchi saba nazo ni Tanzania, Sudan, Nigeria, Eritrea, Kyrgyzstan, Belarus na Myanmar, vyanzo karibu na suala hilo vimesema.
Rasimu ambayo imeandaliwa itaweka masharti ya uhamiaji kwa nchi hizo lakini siyo marufuku ya moja kwa moja kwa raia wa mataifa hayo kuingia nchini Marekani. Masharti hayo huenda yakawakumba maafisa fulani fulani wa serikali, kwa mfano, wale ambao wataomba aina fulani ya visa.
Kwa mujibu wa gazeti la Politico hapa Marekani, masharti yoyote mapya huenda yakaleta mivutano ya uhusiano kati ya Marekani na nchi ambazo zinalengwa, katika mpango huu mpya, ambapo baadhi ya nchi zimekuwa ni mshirika wa Marekani katika mapambano dhidi ya .Baadhi ya mataifa hayo yamekuwa na mahusiano mazuri na Washington katika mapambano hayo ya kigaidi.
Rais Trump katika mahojiano na The Wall Street Journal akiwa Davos, Uswizi kuhudhuria kikao cha uchumi amesema kuwa kuna mataifa zaidi ambayo yatakumbwa na masharti maalum ya kusafiri kuja Markeani, lakini alikataa kutoa orodha ya mataifa hayo.
Msemaji wa White House, Hogan Gidley hakutaka kufafanua zaidi kuhusu mipango ya kuongeza nchi nyingine katika marufuku ya kusafiri, lakini alisema hatua hiyo ambayo awali iliyakumba baadhi ya mataifa yenye waislamu wengi imekuwa na mafanikio makubwa katika “kuilinda nchi yetu na kuongeza wigo wa usalama kote duniani,” ameongeza Gidley.
Trump alitia saini marufuku ya kusafiri kwa wananchi wake kupewa visa kuja Marekani, Januari 27, 2017 wiki moja tu baada ya kuingia madarakani. Amri hiyo awali iliwanyima visa rais kutoka mataifa saba yenye waislamu wengi. Baadhi ya mataifa hayo ni Iran, Libya, Somalia, Syriana Yemen. Chad ilikuwemo lakini iliondolewa katika orodha ya awali.