Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Novemba 28, 2022 Local time: 13:38

Siku saba za TCRA Tanzania kumalizika wiki hii


TCRA ni mamlaka ya mawasiliano Tanzania

Vyombo vya habari vyasema havina hakika na hatima ya urushaji wa matangazo ya nje endapo vitakuwa havijapata vibali vya TCRA wiki hii hata kama tayari vimewasilisha maombi

Wiki hii huenda ikaona vyombo vya habari nchini Tanzania vikawacha kurusha matangazo ya washirika wao wa nje endapo vitakuwa havijapata kibali kutoka Mamlaka ya Mawasiliano, TCRA, baada ya kumalizika muda wa siku saba zilizotolewa na mamlaka hiyo wiki iliyopita.

Hilo linafuatia kanuni mpya za maudhui ya habari zilizotangazwa na TCRA kuvitaka vyombo vinavyoshirikiana na mashirika ya kimataifa kama VOA, BBC na DW kukamilisha utaratibu wa kupata kibali katika muda wa siku saba kwa kuwasilisha maombi na mikataba yao kwa mamlaka hiyo.

Afisa wa TCRA akizungumza na waandishi August 14
Afisa wa TCRA akizungumza na waandishi August 14

Mkuu wa Kitengo cha Leseni za Mawasiliano TCRA Mhandisi Andrew Kisaka ameiambia VOA kuwa mchakato wa kutoa vibali hivyo hautachukua muda mrefu baada ya kuwasilishwa kwa maombi na makubaliano ya vyombo husika.

“Ambaye amekaa kimya na siku saba zimeisha ina maana hakua na mpango wa kuleta makubaliano hayo na atalazimika kusitisha kurusha matangazo hayo kwa maana ataonekana kama tu mvamiaji” ameeleza Mhandisi Kisaka.

Vyombo vinavyorusha matangazo ya nje vinasema endapo vitakosa vibali vya kufanya hivyo itakuwa ni athari kubwa kwa ubora wa matangazo yao kwa jumla. Mkuu wa Vipindi katika Kituo cha radio SAUT jijini Mwanza, Martin Nyoni, anasema ushirikiano na vyombo vya nje ni muhimu kwao kwani licha ya kupata taarifa za habari kutoka nje hupata pia fursa ya kubadilishana ujuzi, hali inayosaidia kuboresha utendaji wao.

Mashirika ya kimataifa “ yana uwezo wa kifedha na kiteknolojia kuweza kufikia matukio kwa haraka, kwa sisi ambao tuko huku ndani ya nchi uwezo wetu katika hayo mawili unatubana kuyafikia matukio yanayojiri ulimwenguni kote, kwa hiyo walaji wetu wa habari watapata taarifa ambazo pengine hazikidhi viwango ambavyo vyombo vya kimataifa vimekua vikitoa” alisema Nyoni

Tangazo la awali la TCRA mapema wiki iliyopita lilikuja kama ongezeko la sheria ya mwaka 2018 na kuzusha taharuki miongoni mwa vyombo vya habari ndani na nje ya nchi na kufanya baadhi ya televisheni na radio kuacha mara moja kurusha matangazo ya washirika wao wa kimataifa.

Kufikia katikati ya wiki TCRA ililazimika kutoa ufafanuzi kadha kuhusu kanuni hiyo mpya na hatimaye kutamka kuwa vyombo vya ndani vinaweza kuendelea kurusha matangazo ya mashirika ya nje lakini yakamilishe utaratibu wa maombi ya kibali katika muda wa siku saba.

Kanuni hizo mpya za TCRA zinasema pia kuwa baada ya kupata kibali cha kurusha matangazo ya shirika la nje mwenye leseni atawajibika kwa maudhui yoyote yasiyozingatia sheria na kanuni hizo. Maafisa wa vyombo vya habari Tanzania wanasema huo utakuwa mzigo usiobebeka kwao.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG