Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Mei 31, 2024 Local time: 01:11

Tanzania: Spika Ndugai amuomba radhi Rais Samia


Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan

Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai, Jumatatu alimuomba radhi Rais Samia Suluhu Hassan na Watanzania “kama hotuba yangu ilimvunja moyo Rais."

Ndugai alikuwa akizungumzia hotuba aliyoitoa wiki jana kuhusu mikopo ya kigeni, ambayo ilionekana na baadhi ya watu kama ya kuleta mgongano kati yake na Rais Samia.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma, Ndugai alisema hakunuia kumkashifu rais kwa njia yoyote ile.

“Kwa hiyo binafsi yangu popote pale ambapo nilihisiwa kwamba nimetoa neno la kumvunja moyo Rais wetu na akavunjika moyo, ninatumia fursa hii kumuomba radhi sana mheshimiwa Rais na Watanzania wote,” Alisema.

“Rais ndio kiongozi wetu mkuu tutamheshimu “aliongeza.

Alisema kuwa hotuba yake ilikuwa inasisitiza ulipaji wa kodi na tozo mbalimbali.

“Katika mazungumzo yale baadaye ikatengenezwa clip na baadhi ya watu wakakatakata mambo, wakawasilisha ujumbe nusu, ujumbe nusu ule umesababisha mjadala mkubwa katika nchi yetu, ambao mjadala umesababisha usumbufu wa hapa na pale,” alisema spika Ndugai

“Kwa hiyo niliona tukutane pamoja na mambo mengine niweke sawa jambo hilo lilivyokuwa, hapakuwa na lolote la kukashifu wala kudharau juhudi zozote za Serikali, tunahitaji Serikali na tunaiunga mkono”

“Katika mazungumzo yetu niliwataka wenzetu pamoja na mambo mengine tulipe kodi, ushuru na tozo mbalimbali huo ndio ulikuwa msisitizo wa hotuba yangu,,” alisema.

Chanzo cha malumbano

Chanzo cha mgongano huo ni kauli zilizotolewa kuhusu mkopo uliopokewa na serikali ya Tanzania kutoka Shirika la Fedha Duniani (IFM) wa shilingi trilioni 1.3, fedha ambazo zinatumika kwa miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa, vituo vya afya na huduma nyinginezo.

Akizungumza jijini Dodoma, Desemba 27, 2021, Job Ndugai alionekana kumlenga moja kwa moja Rais Samia kwa kusema, "Juzi mama ameenda kukopa shilingi trilioni 1.3.

Ndugai alisema: “Hivi ipi bora, sisi Watanzania kwa miaka 60 ya uhuru kuzidi kukopa tuwe na madeni au tubanane hapa hapa, tujenge wenyewe bila madeni haya makubwa yasiyoeleweka. Ni lini sisi tutafanya wenyewe na kwa namna gani? Tutembeze bakuli ndio heshima? Tukishakopa tunapiga makofi, sisi wa kukopa kila siku? Tukasema pitisha tozo anayetaka asiyetaka, pitisha tozo lazima tuanze kujenga wenyewe, nani atatufanyia,yuko wapi huyo mjomba, tukapitisha.”

Aliendele: “Sasa 2025 mtaamua mkitoa waliopo sawa, waje watakaokuwa kazi yao kwenda kukopa, endapo hiyo nayo ni namna ya kuongoza nchi, hivi sasa deni letu ni Trilioni 70. Hivi ninyi wasomi hiyo ni afya kwa taifa? Kuna siku nchi itapigwa mnada hii."

Siku moja baadaye Rais Samia alijibu, na kusisitiza kwamba serikali itakopa kugharamia miradi ya maendeleo.

"Kwa njia yoyote, kwa vyovyote tutakopa.Tutaangalia njia rahisi, njia zitakazotufaa kukopa na fedha hizi hatutazitoa kwenye kodi tunazokusanya ndani, ni lazima tutakopa.

Kama walidhani kutakuwa kuna kusimamishwa miradi ili wapate la kusema, halipo. Kuna jitihada za kutuvunja moyo kwenye mkopo, hakuna nchi isiyokopa, tutakopa tumalize miradi ya maendeleo ili tuendelee kwa sababu ukikopa unajenga sasa kwa haraka na kuharakisha maendeleo na mikopo hii ni ya miaka 20 kwahiyo tutakopa na tutalipa taratibu," alisema Rais Samia.

XS
SM
MD
LG