Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Aprili 18, 2024 Local time: 16:56

Tanzania: Serikali kuondoa marufuku ya mikutano ya kisiasa sio jambo la kusifiwa, ni haki ya wanasiasa - Wachambuzi


Rais Samia suluhu Hassan akihutubia taifa baada ya kula kiapu March 19, 2021
Rais Samia suluhu Hassan akihutubia taifa baada ya kula kiapu March 19, 2021

Wasomi na wachambuzi wa siasa nchini Tanzania wametahadharisha wanasiasa hasa wa upinzani nchini humo, kutofurahia sana hatua ya rais Samia Suluhu Hassan kuondoa marufuku ya shughuli za vyama vya kisaisa.

Wamesisitiza kwamba hakuna haja ya kusherehekea hatua hiyo kwa sababu ilikuwa kosa lililotendwa na serikali iliyopo madarakani kisheria.

Rais samia aliondoa marufuku iliyokuwepo kwa muda wa karibu maiaka sit ana iliyowazuia wanasiasa wa upinzani na vyama vyao kufanya mikutano ya hadhara.

Marufuku hiyo iliwekwa na aliyekuwa rais wa Tanzania wa awamu ya tano hayati John Pombe Magufuli, tarehe 24 June 2016.

Wanasiasa wa chama kinachotawala cha mapinduzi CCM hata hivyo waliendelea kufanya mikutano ya kisiasa wakati wenzao wa upinzani walizuiliwa, kukamatwa na kushitakiwa kwa makosa mbalimbali, yakiwemo ya kupanga kuipindua serikali.

Mengi ya mashtaka hayo yalitajwa kuwa ya kubambikizwa.

Rais Samia amepongezwa kwa kuondoa marufuku

Wanasiasa nchini Tanzania wamekuwa wakieleza kufurahishwa na hatua ya kuondoa marufuku hiyo na kumsifu rais Samia Suluhu Hassan.

Lakini mchambuzi wa siasa na mhadhiri mstaafu katika chuo kikuu cha Dar-es-salaam Professa Xavery Lwaitama, amesema kwamba serikali ilivunja sheria kwa kukiuka haki ya vyama vya kisiasa na kwamba huenda hilo likarudiwa wakati wowote, pasipo kuheshimu demokrasia na katiba ya nchi.

“Maagizo kama hayo yanaweza kutumiwa na polisi kufanya yale yale ya zamani maanake amesema kwamba isiwepo matusi, kukashifiana. Polisi anaweza kutafsiri mtu akikosoa serikali kwamba amekashifu serikali. Hamna kitu chochote cha sherehe hapo. Serikali ya awamu ya sita imejiondoa kwenye kifungo cha uharamu,” amesema prof Lwaitama.

Kiongozi wa upinzani Tanzania Tundu Lissu akihutubia waandishi wa habari mjini Nairobi Kenya, ambapo alipelekwa kwa matibabu baada ya kupigwa risasi kadhaa muda mfupi baada ya kutoka bungeni Tanzania
Kiongozi wa upinzani Tanzania Tundu Lissu akihutubia waandishi wa habari mjini Nairobi Kenya, ambapo alipelekwa kwa matibabu baada ya kupigwa risasi kadhaa muda mfupi baada ya kutoka bungeni Tanzania

Wanasiasa wa Tanzania waliokimbilia uhamishoni

Idadi kamili ya wanasiasa wa Tanzania waliokimbilia uhamishoni wakati wa utawala wa Hayati John Magufuli haijulikani, lakini walioangaziwa zaidi na vyombo vya habari ni kiongozi wa upinzani Tundu Lisu aliyekimbilia Ubelgiji na mbunge Godbless Lema aliyetorokea Canada.

Serikali ya rais Samia imekuwa ikiwahimiza wanasiasa hao kurejea Tanzania.

Wanasiasa waliokuwa wamezuiliwa gerezani kwa ‘mashtaka ya kuwekewa’ kama kiongozi wa chama cha upinzani Freeman Mbowe, aliyefunguliwa mashtaka ya ugaidi baada ya kukamatwa akihutubia wafuasi wa chama chake, wameachiliwa huru.

Rais Samia, katika mojawapo ya hotuba zake mwaka 2022 alisema kwamba waligundua kwamba idadi kubwa ya wafungwa (1840) waliokuwa gerezani walikuwa na kesi za kubambikizwa.

Idadi ya wafungwa waliobambikiziwa kesi za kisiasa haijulikani.

Serikali inastahili kuvumilia ukosoaji ili kukuza demokrasia

Mchambuzi wa siasa Salaam Abdalla ana maoni kwamba kuondolewa kwa zuio la mikutano ya hadhara kwa vyama vya kisiasa ni changamoto nyingine kwa vyama hivyo lakini ni fursa nyingine kwa wanasiasa kuimarisha demokrasia ya Tanzania.

“kwa muda mrefu wamekuwa wakililia zuio hilo liondoshwe. Sasa kuna nafasi kubwa kuonyesha na kueleza wananshi sera zao. Lakini pia ni vyema serikali ifahamu kwamba imefungua milango ya kurekebisha dosari walizokuwa nazo kama serikali na ziwekwe wazi na hadharani pamoja na kupokea maoni ya upinzani kwa kuvumilia.”

Maoni yake Salaam Abdalla yanakaribiana na maoni ya mwanasheria Mbwana Aliamtu anayesema hii ni fursa nzuri kwa vyama vya upinzani kushindana na chama kinachotawala cha CCM.

“Kutakuwa na uwanja sawia kwa kila chama kujiuza kwa wapiga kura, kutoa ubora wake kwa wananchi lakini vipo vyama ambavyo vitapoteza ushawishi na vingine kupotea kwenye dira ya kisiasa.”

Kikao cha Bunge la Tanzania
Kikao cha Bunge la Tanzania

Mabadiliko ya sheria

Wakosoaji wa serikali ya Tanzania hata hivyo wanasema kwamba bunge linahitajika kutekeleza mabadiliko makubwa katika sheria za nchi hiyo na kuweka mazingira ambayo yatazuia kutokea kwa rais kutoa amri zinazobadilishwa na kuwa sheria bila ya kupitia mchakato wa bunge.

Wanataka serikali kuweka mazingira mema yatakayoruhusu raia wa Tanzania kuwa na uhuru wa kuandamana kwa amani, kuwa na uhuru wa kujieleza na kuheshimu haki za msingi za raia.

Sehemu ya 4 ya sheria za bunge za mwaka 1988, zinawaruhusu wabunge kufanya mikutano katika maeneo yao ya bunge pasipo kusumbuliwa. Sheria hiyo vile vile inaagiza serikali kuwapa ulinzi wabunge wanapoandaa mikutano yao.

Tanzania inaendelea na mchakato wa kuandika katiba mpya. Miongoni mwa maswala yenye utata mkubwa ni kupunguza mamlaka ya rais.

Imetayarishwa na Amri Ramadhan, VOA, Dar-es-salaam

XS
SM
MD
LG