Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Oktoba 04, 2024 Local time: 17:31

Tanzania; Rais Samia Suluhu Hassan aongoza maziko ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa

2 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akiweka udongo kwenye kaburi la Waziri Mkuu Mstaafu Hayati Edward Ngoyai Lowassa Monduli Mkoani Arusha.17/2/ 2024. Picha ya Ikulu
2 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akiweka udongo kwenye kaburi la Waziri Mkuu Mstaafu Hayati Edward Ngoyai Lowassa Monduli Mkoani Arusha.17/2/ 2024. Picha ya Ikulu

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameongoza maziko ya aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa taifa hilo Edward Ngoyai Lowassa yaliyofanyika hii leo nyumbani kwake Monduli Arusha na kuudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali pamoja na wanasiasa kutoka vyama vya upinzani.

Akizungumza wakati akitoa salamu za pole kwa familia na wananchi wa Tanzania Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amesema njia nzuri ya kumuenzi hayati Edward Lowassa ni kufanya siasa za maridhiano na siasa za kujenga hoja, kuheshimiana, kustahamiliana bila kulumbana wala kutikisa misingi ya utaifa.

“Hapa tunapata somo kubwa sana la siasa za kujenga hoja, kuheshimiana, kustahamiliana na siasa za kuleta maendeleo huo ni ukomavu mkubwa wa kisiasa na ni njia nzuri ya kuchukua kama tunataka kumuenzi Lowassa na vitendo vyake”

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akiwa pamoja na viongozi wengine katika mazishi ya Waziri Mkuu Mstaafu Hayati Edward Ngoyai Lowassa. 17/2/2024. Picha ya Ikulu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akiwa pamoja na viongozi wengine katika mazishi ya Waziri Mkuu Mstaafu Hayati Edward Ngoyai Lowassa. 17/2/2024. Picha ya Ikulu

Hata hivyo Rais Samia ameongezea kusema kuwa Lowassa ni kiongozi alieacha funzo kuwa watu wanaweza kutofautiana katika mitazamo na sera bila kuvunja misingi ya Utaifa wao.

“alichotufundisha ni kwamba tunaweza tukatofautiana mitazamo, misimamo na sera bila kutukanana kulumbana wala kutikisa misingi ya Utaifa na mshikamano wetu na bado tukaelewana” ameongezea Rais Samia

Kwa upande wa Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani CHADEMA Freeman Mbowe wakati akimuelezea Hayati Edward Lowassa amemtaja kama kiongozi aliyetoa mchango mkubwa katika kuimarisha demokrasia nchini Tanzania na mgombea wa kwanza kutoka upinzani kuonyesha ushindani katika uchaguzi.

Mjane wa Marehemu Mama Regina Lowassa akisali mbele ya jeneza lenye mwili wa Waziri Mkuu Mstaafu Hayati Edward Ngoyai Lowassa nyumbani kwake Monduli Mkoani Arusha. 17/2/2025. Picha ya Ikulu
Mjane wa Marehemu Mama Regina Lowassa akisali mbele ya jeneza lenye mwili wa Waziri Mkuu Mstaafu Hayati Edward Ngoyai Lowassa nyumbani kwake Monduli Mkoani Arusha. 17/2/2025. Picha ya Ikulu

“mheshimiwa Lowassa nae ni muhanga wa mifumo yetu ya uchaguzi lakini huyu alikuwa ni mgombea wa Urais katika upinzani wa kwanza kupata kura zaidi ya million sita halikuwa jambo dogo ni kwasababu ya karama ya huyu mzee”

Mbowe ameongezea kuwa “Nina imani kuwa utendaji kazi kamili wa Mheshimiwa Lowassa haukuwahi kupatikana hivyo tuwape watu nafasi za uongozi katika misingi ya kweli na haki taifa letu likapate viongozi wema ambao watatupeleka mbele wote kwa umoja wetu”

Lowassa aliefariki tarehe 10 ya mwezi februari katika taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete jijini Dar es Salaam ameacha Mjane mmoja Regina Lowassa pamoja na watoto watano kati yao wakiume watatu na wakike wawili.

Imeandaliwa na Amri Ramadhani Sauti ya Amerika.

Forum

XS
SM
MD
LG