Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Oktoba 04, 2024 Local time: 18:04

Tanzania kushirikiana na Korea kusini kujenga bandari ya uvuvi Bagamoyo


Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan. Picha na HANNAH MCKAY / POOL / AFP Nov 2, 2021
Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan. Picha na HANNAH MCKAY / POOL / AFP Nov 2, 2021

Serikali ya Tanzania imetolea ufafanuzi juu ya mkopo iliyopokea kutoka Korea Kusini, ulioambatana na makubaliano ya ushirikiano katika sekta ya uvuvi pamoja na madini.

Kwa mujibu wa Msemaji Mkuu wa Serikali Mobhare Matinyi amethibitisha Tanzania kuingia mkataba na Korea Kusini utakaoiwezesha Tanzania kupokea mkopo wa kiasi cha Dola za kimarekani Billioni 2.5 kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia 2024-2028.

Matinyi amesema kuwa mkopo huo utaanza kulipwa baada ya miaka 25 na utalipwa kwa kipindi cha miaka 40 na hivyo mkopo huo unatarajiwa kuwa mkopo nafuu kutokana na kuwa na riba nafuu ya aslimia 0.01.

“Mkopo huu utaanza kulipwa baada ya miaka ishiri na tano yaani utakapofika mwaka sita kutoka utakapokuwa umemalizika kutolewa 2028 na tutapewa kipindi cha miaka 40 kuulipa tunaposema ni mkopo nafuu maana yake ni kuwa riba ya mkopo huu ni asilimia 0.01” amesema Matinyi.

Matinyi ameendelea kusema kuwa hati za makubaliano zinajumuisha ushirikiano katika uchumi wa bluu ikiwemo masuala ya uvuvi, na utafiti pamoja na ushirikiano katika madini ya kimkakati ikiwemo Nickel, Lithium na Graphite.

Makubaliano hayo yanatarajiwa kuhusisha pia ujenzi wa bandari ya uvuvi Bagamoyo mradi utakaogharimu dola za marekani millioni 156.5 ikiwa ni moja ya sehemu ya miradi ambayo Tanzania inashirikiana na Korea.

“Tunataka kujenga bandari ya uvuvi bagamoyo na ujenzi huu utagharimu jumla ya dola za marekani millioni 156.5 hii ni sehemu ya miradi mingi ambayo uhusiano wetu jamhuri ya korea na Tanzania tumekuwa nao kutoka 2014.”

Hata hivyo Dkt. Bravious Kahyoza ambaye ni mchambuzi wa masuala ya uchumi amesema ni muhimu serikali kuweka utaratibu wa kufanya uchambuzi yakinifu kabla ya kuingia kwenye mikopo kuonyesha namna ambavyo taifa litakwenda kunufaika na mikopo hiyo.

“Serikali ni muhimu kuwa na utaratibu wa kufanya uchambuzi yakinifu na kuonyesha ni kitu gani kinakwenda kutokea, ni kwamba serikali ifanye uchanganuzi makini wa kuonyesha ni kitu gani tunakwenda kukifanya na kitakwenda kutoa matokeo gani kwa umma.” Amesema Kahyoza.

Matinyi amemalizia kwa kusisitiza mkopo huo ni mkopo nafuu na hauna mashariti yoyote yanayohusisha kutoa sehemu ya bahari na madini.

Forum

XS
SM
MD
LG