Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Septemba 28, 2022 Local time: 23:08

Kikwete aombwa kuwawajibisha viongozi wa Ruvuma


Madereve wa pikipiki wamefunga barabara ya Songea kuelekea Tunduru kuelekea afisi ya mkuu wa mkoa wa Ruvuma.

Mtandao wa mashirika ya kutetea haki za binadamu unamuomba Rais Kikwete wa Tanzania kuwawajibisha viongozi wa Ruvuma kwa kile wanachoelezea uzembe uliosababisha mauaji ya raia

Nchini Tanzania kumekuwepo na mtazamo tofauti baina ya makundi mbalimbali kufuatia mauaji ya raia wawili mjini songea mkoani Ruvuma yaliyofanywa na polisi wakati wa maandamano ya wananchi mkoani humo hivi karibuni.Mtandao wa mashirika ya haki za binadamu kusini mwa Afrika - SAHRINGON, tawi la Tanzania umemuomba Rais Jakaya Kikwete kuwawajibisha mkuu wa mkoa wa Ruvuma, mkuu wa Polisi mkoani humo pamoja na mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai wa mkoa huo kwa kile ilichoeleza kuwa uzembe uliosababisha mauaji hayo ya raia katika mjini Songea.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, mratibu wa taifa wa mtandao huo wa mashirika yanayojihusisha na haki za binadamu yapatayo 80 hapa nchini, bibi Martina Kabisama, ameitaka serikali kuwalipa fidia wale wote walioathirika au kupata madhara na hatua hiyo ya askari kuzuia maandamano ya wananchi hatua iliyosababisha vurugu.

Polisi wanawakamata waandamanaji
Polisi wanawakamata waandamanaji


Wakati huo huo kufuatia mauaji hayo ya raia huko Songea, mbunge wa Singida mashariki, Tundu Lissu, ametaka kuundwa kwa tume huru ya kuchunguza tukio hilo.

Akizungumza na Sauti ya Amerika jijini Dar Es Salaam, Ijumaa, bwana Lissu amesema tume hiyo inatakiwa kuundwa na bunge au wadau mbalimbali ili kubaini ukweli huku akipinga vikali uchunguzi huo kufanywa na jeshi la polisi lililohusika katika mauaji hayo.

Hata hivyo wakati Lissu akidai kuundwa kwa kamati huru ya kuchunguza tukio hilo tayari jeshi la polisi limeunda tume yake ya kuchunguza vurugu hizo za songea huku mkuu wa mkoa wa Ruvuma, naye ameunda timu ya watu wanane wa kufanya kazi kama hiyo.

XS
SM
MD
LG