Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Desemba 07, 2025 Local time: 15:47

Tanzania imekopa dola bilioni 2.5 kutoka Korea Kusini


Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan Febrauari 4, 2024. Picha na Tchandrou Nitanga / AFP.
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan Febrauari 4, 2024. Picha na Tchandrou Nitanga / AFP.

Tanzania na Ethiopia zimesaini mikataba kadhaa na Korea Kusini kwa ajili ya kupata mikopo ya mabilioni ya dola kwa ajili ya maendeleo.

Mikopo hiyo itaiwezesha Korea Kusini kupata fursa ya kuchimba madini muhimu katika nchi za Afrika.

Korea Kusini imeandaa kongamano na viongozi 30 wa nchi za Afrika, ikiwemo Tanzania na Ethiopia.

Kongamano linafanyika wiki hii.

Tanzaia imesema kwamba itakopa dola bilioni 2.5 kutoka kwa Korea Kusini katika muda wa miaka mitano ijayo. Mkopo huo utalipwa katika muda wa miaka 40.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan vile vile amesaini makubaliano yatakayoiruhusu Korea Kusini kutumia bahari yake na madini yanayotumika katika teknolojia ya nishati safi kama Nickel, Lithium na Graphite.

Taarifa ya Tanzania imesema nchi hizo mbili zitashirikiana katika utafiti, uwekezaji na uchimbaji pamoja na kuongeza thamani ya madini hayo ya kimkakati.

Ethiopia nayo imesaini mkopo wa dola bilioni 1 utakaolipwa katika kipindi cha miaka minne kwa ajili ya ujenzi wa miundo mbinu, sayansi na teknolojia, afya na maendeleo ya mijini

Serikali ya Tanzania imedai taarifa ya VOA na mashirika mengine ya kimataifa sio sahihi

Bila kutaja mashirika mengine ya habari yaliyochapisha ripoti kuhusu mkopo wa Korea kusini kwa Tanzania, mkurugenzi wa idara ya habari na msemaji mkuu wa serikali Mobhare Matinyi ameitaja VOA moja kwa moja na kudai kwamba taarifa iliyoandikwa na shirika hilo sio sahihi.

“Ufafanuzi huu unafuatia habari yenye dosari iliyorushwa hewani jana na tovuti ya Idhaa ya Kiswahili ya redio ya Sauti ya Amerika (VOA) na kisha kusambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii na kuibua maswali ambayo kwa hakika yanahitaji ufafanuzi wa serikali,” inasema taarifa hiyo ikiongezea kwamba “taarifa hizo pia zimeandikwa na mashirika ya habari ya kimataifa na pia kunukuliwa na magazeti kadhaa nchini Afrika Mashariki zikiwa na upotoshaji.”

Mashirika mengine ya habari yaliyotangulia kuandika ripoti kuhusu mkopo na ushirikiano kati ya Tanzania na Korea kusini ni shirika la habari la Reuters, mshirika wa VOA.

Kulingana na serikali ya Tanzania, mkopo wa dola bilioni 2.5 “ni wa masharti nafuu ambao utatumia miaka mitano kutolewa lakini utaanza kulipwa baada ya miaka 25.”

“Mkopo utakuwa na riba ya asilimia 0.01 kwa muda wote wa malipo,” amesema Matinyi.

Ushirikiano zaidi kati ya Tanzania na Korea Kusini

Serikali vile vile imesema kwamba imesaini makubaliano na serikali ya Korea Kusini ya ushirikiano katika sekta za uvuvi, madini ya kimakati na uanishaji wa majadiliano ya mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi – EPA.

Taarifa ya msemaji mkuu wa serikali vile vile imeorodhesha miradi mingine inayotokana na ushirikiano kati ya Tanzania na Korea Kusini kuwa ujenzi wa hospitali ya Mloganzila, uboreshaji wa hospitali ya taifa ya Muhimbili, bandari ya uvuvi ya Bagamoyo miongoni mwa mengine.

Hata hivyo Tanzania haijatoa ufafanuzi namna Korea Kusini itakavyofaidika na ushirikiano huo au kama Korea Kusini itarudishiwa tu pesa zake ilizotoa kama mkopo na nyongeza ya riba ya asilimia 0.01 pekee kwenye mkopo wa dola bilioni 2.5.

“Serikali ina utaratibu wa kutoa taarifa za ziara za rais mara baada ya kurejea nchini kutoka ziarani ambapo mawaziri husika, watendaji na mkurugenzi wa mawasiliano wa ikulu huzungumza na waandishi.” Amesema mkurugenzi wa idara ya habari na msemaji wa serikali Mobhare Matinyi.

Ripoti hii imeongezwa msimamo wa serikali ya Tanzania na baadhi ya yaliyomo yametafsiriwa kutoka kwa ripoti ya shirika la habari la Reuters.

Forum

XS
SM
MD
LG