Nchi za Afrika zimehimizwa kuchukua tahadhari ya mapema kuyalinda makundi ya watu wa asili vinginevyo tabaka hilo la watu linaweza kutoweka katika uso wa dunia kutokana na mabadiliko ya kasi yanayoendelea kushuhudiwa duniani.
Hayo yamo katika ripoti ya Kamisheni ya Haki za binadamu ya Umoja wa Afrika iliyozinduliwa Alhamisi jijini Dar es salaam Tanzania na kushuhudiwa na makundi mbalimbali ya utetezi wa haki za binadamu.
"Duniani kote siyo tu Tanzania hawa watu wasipopewa ulinzi wa kutosha wasipolindwa na taratibu na mifumo ya sheria za nchi ni jamii ambazo zinaweza kupotea” alisema mtetezi wa haki za binadamu Bw. Onesmo Olenguruma akitolea mfano jamii ya Wahazabe waishio kaskazini mwa Tanzania-Manyara.
Bw.Olenguruma alieleza kuwa jamii ya Wahazabe ni ndogo na inategemea ardhi na uoto wa asili kwa kuendesha maisha yao na maeneo yao yako hatarini kuchukuliwa na wawekezaji.