Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Desemba 07, 2024 Local time: 10:42

Fatma Karume asema hatokata rufaa baada ya kupokonywa uwakili Tanzania


Wakili Fatma Karume wa Tanzania
Wakili Fatma Karume wa Tanzania

Asema hatua ya kumuondoa katika orodha ya mawakili Tanzania Bara imetokana na sababu za kisiasa lakini hana mpango wa kukata rufaa.

Wakili na mwanaharakati maarufu nchini Tanzania, Fatma Karume, amesema kwamba hapangi kukata rufaa baada ya kamati ya mawakili ya Jumuiya ya Mawakili wa Tanganyika kumuondoa katika orodha ya mawakili wa Tanzania bara.

Karume, amesema kwamba ataendelea na uanaharakati katika maswala mbali mbali na hasa kutetea katiba ya Tanzania.

Mapema wiki hii Karume pia alifukuzwa kazi katika kampuni ya uwakili, IMMMA Advocates, ambayo alishiriki katika kuianzisha, kwa madai ya kukiuka maadili kutokana na alivyojiingiza zaidi katika uwanaharakati. Kwa miaka kadhaa Karume amekuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya Rais John Magufuli katika masuala mbali mbali.

Katika mahojiano ya simu na VOA, Karume amesema hatua ya kuondolewa kwenye rejista ya mawakili Tanzania Bara inatokana na sababu za kisiasa na yenye lengo la kumuadhibu kwa kusimamia haki na kutetea katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kulingana na Fatma, masaibu yake yalianza pale alipokosoa uteuzi wa Mwanasheria Mkuu Dkt Adelarus Kilangi aliyeteuliwa na rais John Pombe Magufuli February, 2018.

“Ilianza kwa sababu nilimpeleka Rais Magufuli mahakamani kwa kuvunja katiba ya Tanzania kwa sababu alimteua mwanasheria mkuu ambaye alikuwa hakidhi matakwa ya katiba. Kabla hujakuwa mwanasheria mkuu, unatakiwa uwe umewahi kuhudumu kama mwanasheria wa serikali kwa miaka isiyopungua 15 au uwe umefanya kazi kama mwanasheria wa kujitegemea kwa miaka 15. Kilangi, aliteuliwa kabla ya kufikisha miaka 15 ya kazi ya uwakili,” amesema Fatma Karume.

Kulingana na Karume baada ya kupeleka kesi yake katika mahakama ya rufaa, Mwanasheria Mkuu naye alipeleka malalamiko kwenye kamati ya mawakili kwamba lugha aliyotumia Karume haikuwa nzuri.

Karume amekanusha madai kwamba ana chuki binafsi na rais Magufuli, akisisitiza kwamba ataendelea na harakati za kutetea katiba ya Tanzania bila upendeleo wa aina yoyote.

“Sio Magufuli. Suala kubwa ni kwamba natetea utawala wa kidemokrasia na utawala wa sheria. Ingekuwa sio Magufuli aliye madarakani ni mtu mwingine, ningefanya hivyo hivyo. Agekuwa Tundu Lissu kwa mfano anayefanya hivyo anavyofanya Magufuli, ningefanya hivyo hivyo nikampinga. Kwa sababu ningesema hufuati utawala wa sheria na hufuati katiba yetu. Sio suala la kibinafsi.”

Msimamo wa Jumuiya ya Mawakili

Lakini Rais wa Jumuiya ya Mawakili Tanganyika, Dkt. Rugemeleza Nshalla, amemhimiza Karume kukata rufaa.

Akizungumza na VOA Dkt. Nshalla alisema Karume angetumia nafasi ya kukata rufaa ili suala lake liweze kusikilizwa na jopo la majaji watatu.

“Angekata rufaa ili na sisi tupate mwelekeo mzuri kwa sababu kwenye rufaa ni vitu vingi vitajitokeza na ni majaji watatu wala sio mmoja. Kama chama, tutasoma huo uamuzi kwa uangalifu sana kwa sababu hayo makosa yanaweza kuwa yamemgusa Fatma kwa sasa, lakini yanaweza kuwagusa mawakili wengine.”

Hata hivyo, Karume ambaye ni wakili maarufu Tanzania na binti wa aliyekuwa rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, amesema kwamba hajali na uamuzi uliotolewa dhidi yake na anataka usalie katika kumbukumbu za Tanzania jinsi ulivyo.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Kennes Bwire, Washington DC.

XS
SM
MD
LG