Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Septemba 28, 2023 Local time: 07:12

Ngano kutoka Ukraine imewasili Kenya


Meli ya kubeba nafaka ikipakia chakula katika bandari ya Yuzhe, Odesa, Ukraine. Aug 14, 2022

Meli ya kwanza iliyobeba ngano kutoka Ukraine tangu vita vya Russia vilipoanza imewasili Kenya ikiwa imebeba tani 51,400.

Super Henry, imetia nanga Mombasa, Kenya, inakuwa meli ya kwanza kutoka Ukraine ikiwa imebeba chakula, kuwasili Afrika Mashariki tangu Russia ilipoivamia Ukraine kijeshi Februari 24 mwaka huu 2022.

Meli nyingine mbili zinatarajiwa kuwasili Mombasa hivi karibuni zikiwa na shehena ya tani milioni 78 ya ngano.

Balozi wa Ukraine nchini Kenya Pravednyk Andrii amesema kwamba kuanza kuwasili kwa meli zilizobeba chakula kutoka Ukraine ni hatua muhimu itakayosaidia kukabiliana na uhaba wa nafaka katika mataifa ya Afrika na kumaliza mfumuko wa bei.

“Tunafikiria kwamba chakula kilichowasili hapa hakitoshi na tutaendelea kufanya kazi na viongozi wa Kenya, kampuni za kusafirisha bidhaa ili kuleta ngano na nafaka zaidi ili kukabiliana na uhaba wa chakula nchini Kenya,” amesema Andrii.

Mashambulizi ya makombora yameharibu chakula Ukrainei

Balozi Andrii anasema ingawa wamefaulu kusafirisha nafaka hiyo chini ya mkataba wa kuruhusu meli kusafirisha chakula duniani, ghala na mashamba ya chakula Ukraine yameharibiwa na mabomu ya Russia.

Amekadiria kwamba Russia imesababisha uharibifu wa chakula kinachofikia dola bilioni 4 za Marekani.

Ukraine inataka mataifa ya Afrika kuunga mkono shinikizo la kurefushwa kwa makubaliano ya kusafirisha nafaka kutoka Ukraine yanayokamilika mwezi Novemba.

“Bado tuna akiba ya kutosha ya nafaka kwa sababu kabla ya vita kuanza, tulikuwa na zaidi ya tani milioni 12 ambazo zilikuwa tayari kusafirishwa kuelekea soko la kimataifa. Jumla ya tani milioni 8 za nafaka zimesafirishwa kutoka Ukraine na kufika kwenye masoko ya kimataifa tangu makubaliano yaliposainiwa. Hii ndio maana nawaomba wakenya kutusaidia kushinkiza mkataba huu kuongezewa muda. Lakini changamoto ni kwamba Russia inapinga hatua hii ya kurefusha makubaliano,” amesema balozi Andrii.

Kenya ni mwagizaji mkubwa wa ngano kutoka Ukraine

Balozi wa Ukraine nchini Kenya Andrii Pravednyk akizungumza na waandishi wa habari, Nairobi, Kenya. Feb. 24, 2022.
Balozi wa Ukraine nchini Kenya Andrii Pravednyk akizungumza na waandishi wa habari, Nairobi, Kenya. Feb. 24, 2022.

Kenya iliagiza tani milioni 3 za ngano kutoka Ukraine mwaka 2021.

Kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa zaidi ya watu milioni 4 nchini Kenya wanakabiliwa na ukosefu wa chakula na inatarajiwa kwamba chakula kilichopokelewa leo kutoka Ukraine kitasaidia kupunguza bei ya chakula hasa ngano.

Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Dymto Kuleba alizuru mataifa ya Afrika yakiwemo Kenya, Ghana na Senegal katika ziara ya kidiplomasia na kibiashara.

Mataifa mengi ya Afrika yanategemea chakula hasa nafaka na ngano kutoka Ukraine.

Miongoni mwa mataifa hayo ni Ethiopia, Morocco, Misri Tunisia na Libya.

Imetayarishwa na Collins Adede, VOA, Mombasa

XS
SM
MD
LG