Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Juni 20, 2024 Local time: 21:17

Taliban yatangaza kuundwa kwa serikali mpya ya Afghanistan


Maafisa wa Taliban.
Maafisa wa Taliban.

Taliban Jumanne ilitangaza kuundwa kwa serikali mpya ya mpito itakayoongozwa na Mohammad Hasan Akhund huku Abdul Ghani Baradar akiwa naibu kiongozi.

Katika baraza jipya la mawaziri, Sirajuddin Haqqani, mtoto wa mwanzilishi wa mtandao wa Haqqani, akiteuliwa kama waziri wa mambo ya ndani, msemaji mkuu Zabihullah Mujahid alisema katika mkutano na waandishi wa habari mjini Kabul Jumanne.

Awali, Wataliban wenye silaha walifyatua risasi hewani Jumanne kuwatawanya waandamanaji katika mji mkuu wa Afghanistan wa Kabul, mashahidi wameliambia shirika la habari la Reuters, wakati video inayoonyesha watu wengi wakitoroka, huku milio ya risasi ikisikika, ikisambaa mitandaoni.

Hata hivyo, hakukuwa na ripoti za haraka za majeruhi. Mamia ya wanaume na wanawake waliokuwa wakitoa kauli: "Dumu upinzani," na "Kifo kwa Pakistan" waliandamana barabarani dhidi ya Taliban na kile walichokiita nchi jirani ya Pakistan kuingilia masuala ya Afghanistan.

"Serikali ya Kiislamu inawafyatulia risasi watu wetu maskini," mwanamke mmoja aliyeonekana kufadhaika alisikika akisema, huku milio ya risasi ikisikika, kwenye video hiyo, iliyochapishwa na kituo cha televisheni cha Iran kwenye mtandao wa Twitter.

"Watu hawa (Taliban) hawana haki kabisa, na sio wanadamu hata kidogo,” alisema.

Wakati hayo yakiarifiwa, waziri wa Mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken alisema Jumanne, kwamba Marekani inawasiliana na raia wake wapatao 100, ambao wamebaki nyuma nchini Afghanistan na wanafanya juhudi kuhakikisha ndege za kibinafsi zinaweza kuondoka salama.

Wiki kadhaa kabla ya wanajeshi wa mwisho wa Marekani kuondoka Kabul, vikosi vya kigeni vinavyoongozwa na Marekani vilihamisha wageni wapatao 124,000 na Waafghan waliokuwa katika hatari, lakini dazeni za maelfu, ambao wanaogopa kulipiza kisasi kwa Taliban, waliachwa nyuma.

Akizungumzan na waandishi wa habari katika ziara ya Doha, mji mkuu wa taifa la Mashariki ya Kati la Qatar, Blinken alisema maafisa wa Taliban wameiambia Marekani wataruhusu watu wenye hati za kusafiri waondoke bila matatizo.

XS
SM
MD
LG