Kesi za maambukizi zimekuwa zikiongezeka kwa haraka kwenye taifa hilo la Afrika kusini tangu kutangazwa rasmi kwa kesi ya kwanza mapema mwezi huu, wakati idadi ya vifo ikisemekana kuongezeka maradufu ndani ya muda wa chini ya wiki moja. Waziri wa afya Monica Mutsvangwa wakati akizungumza mbele ya wanahabari baada ya kumaliza kikao cha kila wiki cha baraza la mawaziri, amesema kwamba kufikia Jumanne kesi za maambukizi kote nchini zilikuwa 2,056 na vifo 157.
Mutsvangwa amesema kwamba serikali itaongeza juhudi za utoaji chanjo pamoja na kutumia sheria ya muda itakayoiruhusu kutumia fedha kutoka mfuko wa kitaifa wa dharura, ili kukabiliana na janga hilo. Ameongeza kusema kwamba serikali itashauriana na viongozi wa kimila na kidini kwenye kampeni hiyo, ili kutoa uhamasisho, kwa kuwa wengi walioambukizwa au kufa hawajawahi kupewa chanjo. Hapo awali wizara ya afya ililaumu mikusanyiko ya kidini kwa kueneza maabukizi hayo kwa haraka.