Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Julai 18, 2024 Local time: 14:05

Sura Mpya ya Soko Jipya la Mombasa na Kuinuka kwa Uchumi wa Afrika Mashariki


Sehemu ya Mji wa Mombasa, Kenya
Sehemu ya Mji wa Mombasa, Kenya

Ujenzi wa soko jipya la Kongowea mjini Mombasa ulioigharimu Serikali ya Kenya dola milioni 3.2 za Kimarekani linatarajiwa kuinua kiwango cha uchumi wa taifa sambamba na kuboresha shughuli za wafanyibiashara wadogo wadogo katika jumuiya ya Afrika Mashariki.

Soko hilo limekuwa likihudumia wafanyibiashara kutoka baadhi ya mataifa ya Afrika Mashariki zikiwemo Tanzania na Uganda, na bidhaa zinazouzwa kwa wingi zaidi ikiwa nguo, mboga na matunda.

Licha ya umaarufu wa soko hilo, lawama mbalimbali zimeibuka ikiwa ni pamoja na uchafu wa soko, usimamizi mbaya na ukosefu wa usalama kutokana na idadi kubwa ya watu wanaoingia na kutoka kwenye eneo hilo.

Hali hiyo ilifanya serikali ya Kenya kuchukua hatua ya kurekebisha taswira hiyo kwa kujenga eneo maalum la kufanyia biashara sokoni humo.

Soko hilo jipya linatarajiwa kuwanufaisha wafanyibiashara 1500, lakini kulingana na katibu wa Wizara ya Nyumba na Miundo Mbinu nchini Kenya Bi.Aidah Munano, zaidi ya watu 4000 watafaidika kwa namna mbalimbali.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alizindua rasmi soko hilo mnamo mwezi Agosti mwaka 2016 na kulikabidhi kwa serikali ya jimbo la Mombasa .

Lakini wadau wengi wanaona kuwa changamoto kubwa ni kule kwa soko hilo kutegemea kwa kiasi kikubwa mchango wa wafanyibiashara wa kutoka nchi jirani ya Tanzania wanaoleta biadhaa za mboga na matunda.

Wafanyibiashara hao wanaelezea matatizo wanayo kutana nayo katika mipaka ya Kenya, na pia wanapowasili sokoni humo ambapo wanasema hulipishwa ushuru wa juu kupita kiasi.

“Natoa machungwa Tanzania nakuyaleta hadi Kenya, ninagharimia usafiri lakini nikifika mpakani nalipishwa ushuru mkubwa sana, 21,000/=.

Wengi wao wanasema hayo sio matarajio yao, kwa sababu wanatakiwa waje Kenya wafanye biashara kwa faida ili waweze kurudia mzigo mwingine.” Amesema Bakari Ayubu, mfanyibiashara kutoka Muheza, Tanzania.

Waziri wa biashara jimbo la Mombasa Hamis Mwaguya ameiambia VOA kwamba watakomesha hali hiyo, akiahidi kuwa usimamizi wa soko jipya utahakikisha wafanyibiashara kutoka nje ya nchi wanapewa huduma sawa kama wenyeji wa Kenya.

Mwaguya amesema suala la usalama limetiliwa mkazo katika soko hilo, akiongeza kuwa ukaguzi utakuwa unafanyika kwa kila mtu anaeingia na kutoka kila siku katika soko hilo.

“Tutahakikisha wachuuzi wote wanaoingia sokoni wako na sare rasmi pamoja na vitambulisho. Tunajaribu kuboresha soko hili, na ndio sababu tunafanya kazi kwa karibu na serikali ya kitaifa.” Amesema Waziri Mwaguya.

Soko hilo jipya limejengwa kwa usanifu wa kisasa, likiwa na sehemu ya kuhifadhi mizigo, kupanga bidhaa sehemu wafanyabiashara wanazoshirikiana pamoja na mfumo mbadala wa kutupa na kuhifadhi taka.

Wachuuzi watakaoanza kutumia soko hilo jipya watakuwa wakilipa ada ya Sh.1,200 za Kenya kila mwezi, ambayo ni sawa na Dola 12 za Kimarekani.

XS
SM
MD
LG