Waziri Mkuu wa Sudan, Abdalla Hamdok yuko kwenye kizuizi cha nyumbani katika kile kinachoonekana kuwa mapinduzi kulingana na ripoti za televisheni nchini humo.
Msaidizi wa Waziri Mkuu alisema jeshi linahusika na mapinduzi ya Jumatatu kulingana na ripoti wakinukuu vyanzo vya familia, shirika la habari la Reuters, liliripoti kwamba vikosi vya jeshi vilivamia makazi ya Waziri Mkuu mapema Jumatatu.
Mawaziri wanne wa baraza la mawaziri na mwanachama mmoja wa kiraia wa baraza kuu linalotawala pia walikamatwa, televisheni ya Al-Hadath iliripoti. Viongozi wa chama na maafisa wengine wa serikali pia wamekamatwa, huku huduma ya internet katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum imevurugika kulingana na waandishi wa habari pamoja na wanaharakati waliopo huko. Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Sudan pia umefungwa.
kwa mujibu wa shirika la habari la AP na picha zilizoonekana kwenye mitandao ziliwaonyesha waandamanaji wakiziba barabara na kuchoma moto matairi wakati vikosi vya usalama vilitumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya.
Waandamanaji walisikika wakipiga kelele “watu wana nguvu na kujiweka kando siyo njia mbadala” huku moshi ukitanda hewani. Jeshi kuchukua madaraka itakuwa ni kikwazo kikubwa cha kurudi nyuma kwa Sudan ambayo imekabiliwa na mabadiliko mengi na huku ikisonga mbele katika kipindi cha mpito kuelekea demokrasia tangu mtawala wa muda mrefu Omar al-Bashir alipopinduliwa nchini humo kufuatia maandamano makubwa miaka miwili iliyopita.