Rais wa Sudan Omar al-Bashir anasema nchi yake itatoa sarafu mpya kufuatia kujitenga kwa upande wa kusini wiki iliyopita. Rais Bashir alitangaza mpango huo alipohutubia bunge mjini Khartoum Jumanne.
Sudan Kusini ilitangaza uhuru wake rasmi Jumamosi iliyopita na Jumatatu ikatangaza mipango ya kuwa na sarafu yake mpya.
Sarafu mpya ya Sudan Kusini inategemewa kuwasili kwa ndege ya mizigo kutoka Uingereza Jumatano na kuanza kuingizwa kwenye mzunguko wa fedha Jumatatu ijayo.
Haikujulikana mara moja ni wakati gani Sudan (Khartoum) itakuwa na sarafu mpya.