Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Aprili 17, 2024 Local time: 14:07

Sudan Kusini yakaribisha uhuru wake


Raia wa Sudan Kusini wakisherehekea uhuru wao Julai 9 mjini Juba
Raia wa Sudan Kusini wakisherehekea uhuru wao Julai 9 mjini Juba

Maelfu ya raia wa Sudan Kusini washerehekea uhuru wao, matunda ya miaka zaidi ya 20 ya mapambano

Maelfu ya watu wamekusanyika katika mji wa Juba mji mkuu wa Sudan Kusini leo Jumamosi kusherehekea uhuru wa taifa jipya kabisa duniani. Sudan Kusini ilibadilika na kuwa taifa jipya ilipofika saa sita usiku Ijumaa saa za Afrika Mashariki na wakaazi wengi wa mji wa Juba kumiminika mitaani wakicheza densi kukaribisha taifa lao jipya.

Spika wa bunge la Sudan Kusini James Wani Igga alitangaza rasmi uhuru wa nchi hiyo mpya katika hotuba yake. Rais wa Marekani Barack Obama ametangaza kuwa Marekani inatambua rasmi taifa hilo jipya.

Miongoni mwa wageni mashuhuri waliohudhuria sherehe hizo ni Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon na viongozi wengine 30 wa nchi akiwemo rais wa Sudan Omar al-Bashir. Rais wa Kenya Mwai Kibaki alikuwa wa kwanza miongoni mwa wageni walioalikwa kutoa hotuba kutambua taifa hilo jipya la Sudan Kusini.

Sudan Kusini ilipiga kura ya maoni na kuamua kwa wingi wa kura kujitenga na Sudan Kaskazini katika kura iliyofanyika Januari mwaka huu. Maamuzi ya kufanya kura hiyo yalifikiwa katika mkataba wa amani wa mwaka wa 2005 uliohitimisha zaidi ya miaka 20 ya mapigano ya wenyewe kwa wenyewe baina ya watu wa Kaskazini na Kusini mwa Sudan.Sudan Kaskazini ilitoa tangazo rasmi kutambua taifa hilo jipya Ijumaa kupitia televisheni ya kitaifa.

Na kwa mara ya kwanza bendera mpya yenye rangi sita ya Sudan Kusini imepandishwa, na rais Salva Kiir kuapishwa kuwa rais wa kwanza wa taifa hiloi. Sherehe za leo Jumamosi mjini Juba zimefanyiwa katika uwanja wa John Garang uliopewa jina la kiongozi wa waasi wa Sudan Kusini aliyekuwa mstari wa mbele kupigania uhuru wa upande wa kusini mwa Sudan. Garang alifariki katika ajali ya helikopta mwaka wa 2005.

Marekani imewakilishwa na maafisa wa ngazi ya juu katika sherehe hizo akiwemo balozi wake katika Umoja wa Mataifa Susan Rice, mjumbe maalum kwa Sudan Princeton Lyman na waziri wa zamani wa mambo ya nje Colin Powell.

XS
SM
MD
LG