Mwaka huu, hali ya ukosefu wa usalama wa chakula utawaathiri zaidi ya watu milioni saba , takriban asilimia 60 ya idadi ya watu nchini humo, kama hawatapatiwa msaada wa endelevu inasema Umoja wa Mataifa.
Ripoti ya pamoja ya mashirika matatu ya Umoja wa Mataifa yanasema kwamba hivi sasa, takriban nusu ya idadi ya watu wako katika kiwango cha “mzozo” kwa ukosefu wa usalama wa chakula tangu mwezi Januari.
Serge Tissot, mwakilishi wa shirika la Chakula na Kilimo kwa Sudan Kusini, anasema hali inazidi kuwa mbaya zaidi kutokana na kupanuka kwa mzozo.
“Hata kwa kuwapatia msaada wa kibinadamu, bado tuna watu milioni 1.9 ambao wanakaribia sana kukumbwa na njaa,” amesema Tissot.
Baadhi ya sehemu za Sudan Kusini zimetangazwa kuwa ni maeneo yenye njaa tangu mwanzoni mwa mwaka 2017. Umoja wa Mataifa umeonya kwamba hali kama ya njaa huenda ikarejea wakati wa msimu wa mavuno machache, Mei mpaka Julai, kama misaada ya kibinadamu haitapewa fursa ya kuwafikia walengwa na kuendelea kutolewa.
Kujitayarisha kwa hali hiyo, Idara ya Umoja wa mataifa ya Mpango wa Chakula Duniani inajiweka tena sawa kwa kuyataja maeneo yanayohitaji chakula ambayo huenda yakawa shida kuyafikia wakati wa mwanzo wa msimu wa mvua mwezi April. Idara hiyo pia inapanga kugawa asilimia 20 zaidi ya chakula kuliko mwaka jana, baadhi ya tani 140,000 katika zaidi ya maeneo 50.
Vita vya wenyewe kwa wenyewe vilipozuka Sudan Kusini Desemba mwaka 2013 na hivyo kuwalazimisha watu milioni mbili kukimbia nchini. Wengine milioni mbili wamekoseshwa makazi ndani ya nchi, na wengi wao wanashindwa kupanda chakula chao.
Crystal Wells ni msemaji wa kanda wa kamati ya kimataifa ya msalaba mwekundu (ICRC) yenye makao yake mjini Nairobi. Anasema mashirika ya misaada mara kwa mara yanakabiliana na hali ya dharura kwa kugawa chakula cha misaada kwa watu wasiokuwa na makazi na huduma za afya kwa majeruhi wa vita.
Wells anasema, “ni moja ya majibu yetu makubwa duniani na ndiyo sababu mahitaji ni makubwa sana. Kwahiyo, ni muhimu sana kwamba jamii ya kimataifa inaendelea kutoa msaada kwa taasisi za kibinadamu kama vile ICRC kwasababu kimsingi mara nyingi ni tofauti iliyopo ni kati ya maisha na kifo.”
Tissot wa Umoja wa Mataifa anasema ana imani kuwa misaada ya kimataifa itazuia njaa kuibuka tena nchini Sudan Kusini. Lakini anaelezea kuwa msaada wa chakula kwa nchi, kiasi dola bilioni 1.7 kwa mwaka, hazitoshi.
“Suluhisho siyo tu kupitia ugawaji chakula. Suluhisho la kwanza ni lazima liwe kupitia mkataba wa amani na ukarabati wa sekta ya kilimo nchini Sudan Kusini,” amesema Tissot.
Mzozo ukiingia mwaka wake wa tano, suluhisho la aina hiyo halionekana linakaribia kupatikana.