Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Julai 27, 2024 Local time: 04:11

Upinzani wa Sudan Kusini wasikitishwa na maoni ya mkuu wa majeshi


Kiongozi wa uasi wa Sudan Kusini, Riek Machar akizungumza na waandishi wa habari katika makazi yake mjini Addis Ababa, Ethiopoia akielezea kukubali uteuzi wa Rais Salva Kiir wa kuwa makamu wa kwanza wa rais.
Kiongozi wa uasi wa Sudan Kusini, Riek Machar akizungumza na waandishi wa habari katika makazi yake mjini Addis Ababa, Ethiopoia akielezea kukubali uteuzi wa Rais Salva Kiir wa kuwa makamu wa kwanza wa rais.

Kundi la upinzani nchini Sudan Kusini limesema maoni ya karibuni yaliyotolewa na mkuu wa majeshi ya nchi hiyo ni dhidi ya amani na demokrasia.

Wiki iliyopita mkuu wa majeshi, Paul Malong Awan amesema kwa kipindi ambacho atakuwa hai, makamu rais wa zamani na kiongozi wa uasi, Riek Machar kamwe hatakuwa rais wa taifa hilo jipya duniani.

Akiongea wakati wa ziara yake kijijini kwake Malualkon, Jenerali Awan hakusema jinsi atakavyomzuia kiongozi wa kisiasa wa upinzani kuwa rais.

Msemaji wa Machar, James Gatdet Dak ameshutumu maoni ya Awan kuwa ni ukumbusho mbaya kwamba bado kuna maafisa waandamizi wa kisiasa na kijeshi katika serikali huko Juba ambao hawataki amani na demokrasia.

Maoni ya Awan yamekuja baada ya Machar kutangaza mipango ya kurejea Juba hapo Aprili 18 kuchukua wadhifa wake wa makamu wa kwanza wa rais ili kuunda serikali ya mpito kwa mujibu wa mkataba wa amani wa mwaka 2015 ambao umemaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vya zaidi ya miaka miwili.

Uchaguzi ikiwemo kinyang’anyiro cha urais kwa mujibu wa mkataba wa amani, utafanyika katika mwisho wa kipindi cha miezi 30 cha serikali ya mpito.

Dak amesema Awan hana haki ya kumnyima raia au kiongozi yoyote haki yake ya kuwania nafasi ya urais wa Sudan Kusini

XS
SM
MD
LG