Maafisa wa wizara ya afya nchini Sudan kusini walisema wanalazimika kutupa dozi elfu sitini za chanjo ya kupambana na ugonjwa wa Covid-19 kutoka kampuni ya Oxford na AstraZeneca kufuatia matatizo yanayotokana na dawa hiyo na wasi wasi uliozuka miongoni mwa wananchi.
Dawa hiyo ilitolewa kama msaada na kampuni ya mawasliano ya MTN na Umoja wa Afrika mwezi Machi. Richard Lako msimamizi wa Covid-19 katika wizara ya afya ya Sudan Kusini alisema walipopokea chanjo hizo waligundua baadae kwamba ni lazima zitumiwe katika muda wa siku 14 vinginevyo zitakua zimepitwa na muda. Lako alisema hivi sasa wanafanya mipango ya kutupa chanjo hizo.
Sudan Kusini ilipokea dozi zingine laki moja na elfu 32 za dawa hiyo mwishoni mwa mwezi Machi chini ya mpango wa kimataifa wa COVAX lakini mpango wa kuwapa watu chanjo umecheleweshwa na hadi wakati huu anasema ni watu elfu mbili peke waliopatiwa chanjo.