Makamu Rais wa Sudan, Ali Osman Taha, amewaomba wanachama wenzake wa Umoja wa Mataifa kuisamehe nchi yake deni la nje la dola bilioni 38, kabla ya kura ya maoni ya mwezi Januari huko Sudan kusini.
Taha aliuambia mkutano wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa huko New York, kwamba kufutwa deni hilo kutasaidia kupambana na misukosuko ambayo inaleta ukosefu wa uthabiti nchini Sudan.
Shirika la fedha duniani- IMF linasema Sudan imelegea katika kulipa madeni yake na kwamba haistahili kupunguziwa mzigo wa madeni wala kupewa mikopo zaidi.
Eneo la Sudan Kusini lenye utajiri wa mafuta litapiga kura Januari 9 mwakani kuamua ikiwa itajitenga na kuwa nchi huru au kubaki katika serikali ya kushirikiana madaraka na upande wa Kaskazini.
Kura hiyo ni sehemu ya makubaliano ya amani yaliyomaliza miongo kadhaa ya vita vya wenywe kwa wenyewe nchini humo.