Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Julai 14, 2024 Local time: 13:44

Spika wa Bunge la Kenya aamuru kutotangaza wazi viti vya wabunge waliotoroka vyama vyao.


Wabunge wa Kenya wakiheshimisha kanuni za kutokaribiana bungeni, kutokana na janga la Covid 19. Juni 10, 2021.Picha ya Reuters.
Wabunge wa Kenya wakiheshimisha kanuni za kutokaribiana bungeni, kutokana na janga la Covid 19. Juni 10, 2021.Picha ya Reuters.

Wabunge wa Kenya waliohama vyama vyao vya kisiasa vilivyowapeleka bungeni wamepata afueni baada ya spika wa bunge la kitaifa Justin Muturi kuamuru kuwa hatatangaza wazi viti hivyo, licha ya sheria kumtaka kufanya hivyo.

Vyama vya kisiasa nchini humo vimekuwa vikieleza kuwa vitawafurusha wabunge waasi waliotangaza wazi kuondoka kwenye vyama vilivyowapeleka bungeni na kushabikia sera za vyama vingine.

Spika Muturi amesisitiza kuwa hakuna mbunge hata mmoja aliyemwandikia karani wa bunge kuhusu uamuzi wake wa kuhama chama kilichompeleka bungeni humo.

Muturi, ameeleza kuwa jaji wa mahakama kuu—ambayo ni mahakama ya kikatiba, Joel Ngugi alitoa maamuzi ya kisheria yanayowashinikiza maspika wa bunge la Kenya na mabunge ya serikali za majimbo kutotangaza wazi viti vya wabunge walioondoka kwenye vyama vyao vilivyowapeleka bungeni, licha ya kuwa watoro katika vyama hivyo.

Muturi, ameongeza kuwa karani wa bunge la Kenya hajapokea wasilisho lolote kutoka kwa mbunge yeyote kutaka kuhama rasmi kutoka chama chake cha kisiasa kilichomwingiza bungeni na hivyo basi hawezi kutangaza nafasi hizo wazi.

“Hakuna aliyeniandikia barua kuonyesha kuwa amejiuzulu. Kwa nini nichukue nafasi ya mpelelezi? Na kama jumba la rekodi tunafaa pia kufahamu tahadhari ya mahakama kuhusu agizo lililotolewa na Jaji wa Mahakama kuu Joel Ngungi”, amesema.

Kifungu cha 14(a) cha Sheria ya vyama nchini Kenya kinaweka masharti ya kujiuzulu ambayo ni pamoja na kwamba mwanachama atahesabika kujiuzulu iwapo mwanachama huyo pamoja na mambo mengine, ataunda chama kingine cha kisiasa au kujiunga na chama kingine kando na kilichompa nafasi kuingia bungeni.

Tangazo hili la Muturi ni afueni kwa wabunge wengi nchini Kenya hasa kutoka chama tawala Jubilee ambacho idadi nyingi ya wabunge wake wamebadili chama kutokana na mabadiliko ya mienendo ya kisiasa na kujiunga na chama cha Wiliiam Ruto, United Democratic Alliace, anachotumia kugombea urais, katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Ripoti imeandaliwa na mwandishi wa Sauti ya Amerika mjini Nairobi, Kennedy Wandera.

XS
SM
MD
LG