Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 26, 2024 Local time: 09:55

Somalia: 'Daktari' wa al-Shabaab ahukumiwa kifo


FILE - Wapiganaji wa al Shabaab wakiwa katika gari aina ya pickup wakielekea Mogadishu, Somalia, Dec. 8, 2008.
FILE - Wapiganaji wa al Shabaab wakiwa katika gari aina ya pickup wakielekea Mogadishu, Somalia, Dec. 8, 2008.

Mohamed Abdi Jirow, ambaye pia anajulikana kama ‘Dr Fanah’ alihukumiwa adhabu ya kifo na mahakama ya kijeshi mjini Mogadishu iliyokuwa ikisikiliza kesi hiyo iliyomalizika Januari 14.

Ikitangazwa adhabu ya kifo siku ya Alhamisi, mahakama ilisema, imemkuta na hatia mshtakiwa kwa kuhusika na njama mbalimbali dhidi ya maafisa wa serikali na raia kwa miaka mingi.

Jirow alikiri kutumia aina mbalimbali za utambulisho kwa udanganyifu, ikiwemo kujitambulisha kama daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa neva. Pia alikuwa na sare za kijeshi zilizokuwa na cheo cha ‘meja’

“ Kama njia ya udanganyifu, nilitumia taaluma na vitambulisho mbalimbali kikiwemo cha ‘Dr Fanah’ daktari bingwa, na meja wa jeshi, vitambulisho viwili kutoka zahanati na wizara ya afya na huduma za jamii ya Somalia” amesema ‘Daktari Fanah’ kama alivyonukuliwa kwenye hati za mahakama.

Mpiganaji wa al Shabaab amesema alikuwa akimiliki jumla ya vitambulisho vitano kikiwemo cha UNDP. Alitumia fursa ya Somalia kutokuwa na mfumo wa vitambulisho unaokubalika kitaifa, ambao unawawezesha raia kutumia utambulisho tofauti.

“Niliandaa kadi zote hizo ili kuvipotosha vyombo vya usalama vya serikali,” alidai kufanya hivyo.

Mahakama ilibaini kuwa Jirow alihusika na operesheni mbalimbali ambazo zilisababisha vifo vya watu wengi. Katika kipindi cha televisheni kilichorushwa na Televisheni ya Taifa ya Somalia (SNTV), inayomilikiwa na serikali, Jirow alidai alipanga shambulio la kujitoa mhanga dhidi ya wajumbe waliowakilisha wa mikoa ya kaskazini magharibi wakati wa uchaguzi wa wabunge mwaka 2022.

Shambulio la ngazi ya juu la Eel-Gaab, katikati ya mji wa Mogadishu lilifanywa na watu waliokuwa wamevaa vilipuzi.

“Nilipanga shambulio hilo na niliwapeleka washambuliaji katika eneo la Eel-Gaab, (Mogadishu),” amekiri Jirow.

Mahakama ilitangaza kuwa Jirow alikamatwa akiwa mjini Beledweyne, kilometa 335 kaskazini mwa Mogadishu, baada ya kutiliwa mashaka akiwa amevaa sare za jeshi zilizomtambulisha kuwa meja wa jeshi.

Mahakama ilifahamu kuwa Jirow mwenye umri wa miaka 27, alijiunga na Al-Shabaab mwaka 2007.

Chanzo cha habari hii ni gazeti la "The East African" linalochapishwa Kenya.

XS
SM
MD
LG