Soko hilo la miongo mingi sana litakuwa kivutio kwa wafuasi milioni moja wa kandanda wanaotarajiwa kwenye michuano hiyo itakayoanza Novemba 20.
“Kutakuwa na umati mkubwa wa watu, hatujawahi kuona jambo kama hili," alisema Abdul Rahman Mohammed Al-Nama, mkuu wa mazizi kwenye soko hilo ambaye huwaandaa ngamia na farasi kwa ajili ya wale wanaotaka kuwapanda. "Inshallah (Mungu akipenda), tuko tayari” alisema.
Umati wa watu tayari unaongezeka huku gumzo la Kombe la Dunia likiongezeka.
Vivutio vya mashabiki na vibanda vya muda vya biashara vinafunguliwa na mamia ya maduka madogo madogo yanayouza udi, viungo, mazulia, dhahabu na hata wanyama. Baadhi ya sehemu kwenye soko hilo limejaa mitandio, bendera na kofia zilizoandikwa majina ya mataifa 32 yanayoshiriki mashindano.
Ripoti za vyombo vya habari zilisema maduka yataruhusiwa kufunguliwa kwa saa 24 kwa siku wakati wa Kombe la Dunia.
Mashabiki wa kigeni "watakuwa na furaha tele", alisema Yasmine Ghanem, mchezaji wa timu ya taifa ya wanawake ya gofu ya Qatar, mwenye umri wa miaka 28, ambaye alikuwa ameketi katika mgahawa huko Souq Waqif akinywa kahawa na kula chapati (pancakes). "Itakuwa mchanganyiko mkubwa wa utamaduni wa Kiarabu na soka," aliongeza.
Kila jioni, maeneo yanajaa watu wanaokunywa kahawa na kuvuta Shisha ni eneo lisilo na pombe. Lakini wafanyabiashara, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakijiandaa kwa Kombe la Dunia, wanatarajia mengi zaidi.
Mabilioni ya dola yametumika katika usafiri wa treni mpya pamoja na miundo mbinu ambayo imelipa jiji mabadiliko makubwa na hoteli nyingi mpya pia zimejengwa.
Taifa hilo linataka kutumia Kombe la Dunia kuimarisha kampeni ya kuongeza idadi ya wageni kutoka milioni 1.5 kwa mwaka hadi milioni sita ifikapo mwaka 2030.
Mtendaji mkuu wa Qatar Airways Akbar Al Baker alisema kampuni yake inawekeza "mamilioni ya dola" kwenye miundo mbinu mipya na kukuza utalii.
Kombe la Dunia litakuza tu na kuongeza mtazamo unaobadilika ambao watu wanaweza kuwa nao kwa sasa kuhusu Doha na Qatar,” alisema Kamilla Swart-Arries, Profesa mshiriki katika michezo na utalii katika Chuo Kikuu cha Hamad bin Khalifa.
Katika saa ya kuhesabia ya Kombe la Dunia kwenye barabara ya Corniche iliyo mbele ya bahari, Wabangladeshi, Wahindi, Wanepal, Wapakistani, Wakenya na Waganda kutoka jumuiya kubwa ya wahamiaji ya Qatar humiminika kupiga picha za Selfie karibu na jengo la kisasa.
“Mimi ni shabiki wa Lionel Messi na nina tiketi ya kuona Argentina ikicheza na Saudi Arabia," alisema Anwar Sadath, 56, mhasibu wa India." Litakuwa tukio la kukumbukwa.”
Souq Waqif ilipofunguliwa mwanzoni mwa karne ya 20, wafanyabiashara walisimama mlangoni wakiwapigia kelele wapita njia kununua bidhaa zao. Jina lake linamaanisha "soko la kusimama”.
Ukiwa umeharibiwa na moto mkubwa wa mwaka 2003, sehemu yake kubwa imejengwa upya kwa vichochoro vya waenda kwa miguu kama sehemu ya mradi wa kutengeneza upya eneo la kati la Doha.