Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Machi 28, 2024 Local time: 14:55

Simone Gbagbo ahukumiwa miaka 20 jela


Rais wa zamani wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo na mkewe Simone Gbagbo wakati mumewe alipokuwa madarakani
Rais wa zamani wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo na mkewe Simone Gbagbo wakati mumewe alipokuwa madarakani

Mke wa rais wa zamani wa Ivory Coast, Simone Gbagbo amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa kushiriki kwake katika ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2011.

Mahakama moja mjini Abidjan siku ya Jumanne ilimkuta na hatia bibi Gbagbo ya kudumaza usalama wa nchi na kuandaa magenge yenye silaha katika ghasia ambazo zilisababisha vifo vya watu 3,000. Yeye na mumewe Laurent Gbagbo walishindwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 ambao ulimpatia ushindi mpinzani wa Gbagbo, Alassane Ouattara.

Mwendesha mashtaka wa serikali Soungalo Coulibaly alisema “tunaona kwamba kufanya mambo bila ya kuhofia kushtakiwa hayawezi kuendelea nchini Ivory Coast”. Wafuasi wa Gbagbo walisema kesi hiyo ilikuwa na ushawishi wa kisiasa.

Hukumu hiyo ya mke wa rais wa zamani nchini Ivory Coast ni mara mbili ya muda uliopendekezwa na waendesha mashtaka wa kifungo cha miaka 10.

Mtoto wa kiume wa rais wa zamani wa Ivory Coast, Michael Gbagbo pia alihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela kwa kushiriki kwake katika ghasia hizo.

Laurent Gbagbo baada ya kukamatwa 2011
Laurent Gbagbo baada ya kukamatwa 2011

Wakati huo huo Laurent Gbagbo anasubiri kesi yake kwenye mahakama ya kimataifa ya uhalifu-ICC mjini The Hague kwa shutuma za uhalifu wa vita ikiwemo mauaji, ubakaji na kuwashtaki wapinzani wa kisiasa.

Mwezi Disemba mahakama ya kimataifa ya uhalifu-ICC ilisema Ivory Coast lazima imkabidhi mke wa rais wa zamani wa nchi hiyo anayekabiliwa na mashtaka ya mauaji ya halaiki kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

Serikali ya Ivory Coast ilikataa amri kutoka ICC ya kumkabidhi Simone Gbagbo anayekabiliwa na mashtaka sambamba na hayo.

Bwana Gbagbo aliongoza Ivory Coast kwa zaidi ya muongo mmoja kabla ya kuondolewa madarakani na kukamatwa na majeshi yanayomuunga mkono Ouattara yaliyosaidiwa na Ufaransa hapo mwezi April mwaka 2011.

XS
SM
MD
LG