Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Juni 16, 2024 Local time: 14:32

Mawaziri wa Tanzania wataka ushahidi wa utekaji nyara raia


Zitto Kabwe
Zitto Kabwe

Maelezo zaidi juu ya madai ya watu kutekwa nyara nchini Tanzania yameendelea kujitokeza Jumanne huko katika kikao cha Bunge kinachoendelea Dodoma.

Vyanzo vya habari huko Dodoma vinasema kuwa tayari kadhia hiyo imechukua sura mpya wakati Waziri katika Ofisi ya Rais (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa) George Simbachawene alipowataka wabunge ambao wanaihusisha Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) na utekaji nyara huu wa siri kujitokeza na ushahidi kamili.

Malumbano yazidi

Kwa mara nyingine Bunge limeshuhudia malumbano mazito baada ya mbunge wa Kigoma mjini Zitto Kabwe kudai kuwa anataarifa kuwa TISS ndio imehusika na kutoweka kwa mwanachama wa Chadema Ben Saanane, ambaye kupotea kwake kumebakia kuwa ni siri nzito mpaka hivi leo.

“Kwa mujibu wa Sheria ya usalama wa taifa, inakataza TISS kusimamia utekelezaji wa sheria, kwani chombo hiki hakijapewa mamlaka kukamata, hata kama wakimuona mwizi… Sheria inawakataza,” Zitto ameeleza.

Kutokana na shinikizo la Zitto, Simbachawene ambaye maelezo yake yaligusia usalama wa nchi, alisimama na kumuomba mwenyekiti kuwaamrisha wabunge kuleta ushahidi juu ya TISS kuhusika mbele ya Bunge ili hatua zaidi zichukuliwe.

Mwiko Kuizungumzia TISS

Simbachawene amekumbusha kuwa ni mwiko kuzungumzia mambo yanayohusiana na shughuli za taasisi ya usalama wa taifa, ndani ya bunge au kukishutumu chombo hicho kwa matukio ya utekaji nyara bila ya kutoa ushahidi.

“Mbunge anajua wazi kwamba kile anachozungumza kinakatazwa kuzungumziwa hapa, anazungumzia suala la usalama wa taifa jambo ambalo haruhusiwi kulizungumzia katika bunge, lakini pia anaituhumu TISS kuhusika na utekaji huo, anaweza kuthibitisha hilo katika bunge hili?”

“Na kwa kuwa anajua ni makossa kufanya hivyo … na ni mwiko… Bado, ameendelea hadi hapo na kutuhumu kitu ambacho sina uhakika kama ana ushahidi wa kutosha, kwa hivyo nauliza, kwa ruhusa yako mwenyekiti, Zitto atalazimika kuleta ushahidi Bungeni kwamba TISS wamemshikilia mateka Ben Saanane,” Simbachawene alijibu tuhuma hizo kama sehemu ya maelezo yake.

Hussein Bashe atoa ushuhuda

Baada ya maelezo ya waziri, mbunge wa Nzega Hussein Bashe alijibu kauli ya waziri kwa kutoa undani wake zaidi, hali akiwa na mshangao mkubwa, akidai kuwa yeye ni kati ya wale watu waliofikwa na utekaji huo unaodaiwa kuendeshwa kwa siri na baadhi ya maafisa wa usalama wa taifa.

“Ninapenda kumfahamisha Simbachawene ambaye ni waziri kuwa mimi Hussein Mohamed Bashe… Nilitekwa na maafisa wa usalama wa taifa,” amesema Bashe.

Bashe alianza kujieleza kwa upole na mara alipandwa na dukuduku na kwa ghadhabu aliwatuhumu baadhi ya wabunge: “Acheni kuwa wanafiki… Acheni unafiki, sisi sote ni watanzania… mimi ni mwanachama wa CCM… Sijali iwapo unataka kunivua nafasi yangu ya ubunge.

Hata hivyo juu ya kwamba Zitto alikubali kuwa ni utamaduni potofu kujadili TISS bungeni, aliahidi kufikisha ushahidi “iwapo atatakiwa kufanya hivyo na kamati teule ya bunge.”

Mbunge aomba muongozo

Mapema kabla ya hapo, mbunge wa Iringa mjini (Chadema), Peter Msigwa aliomba muongozo wa kiti, akipendekeza kuwa bunge liruhusiwe kujadili matukio haya ya utekaji wa siri unaoendelea nchini.

Katika kujibu suala la utekaji Waziri Jenista Mhagama kinara wa bunge alimshauri mwenyekiti kuwaruhusu wabunge wenye ushahidi kupeleka ushahidi wao ili bunge liufanyie kazi.

Kwa upande wake Mwenyekiti Mussa Azzan Zungu ameahidi kufikisha mgogoro huo kwenye kamati ya uongozi ya Bunge kwa ajili ya kuchukuliwa hatua.

Wakati anachangia bajeti ya waziri mkuu, mbunge wa Chalinze Ridhiwani Kikwete amesema: “Alikuwa ameshangazwa na ukimya wa waziri wa mambo ya ndani Mwigulu Nchemba juu ya kuwepo malalamiko yanayotoka kwa wananchi kuhusu taarifa za utekaji nyara raia – akimtaka ajitokeze na kuweka wazi kile kinachoendelea kwa upande wa serikali.”

XS
SM
MD
LG