Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Oktoba 05, 2024 Local time: 14:48

Shule zote Kenya zimefungwa kwa ajili ya uchaguzi mkuu


Wanafunzi wa shule ya upili ya Makongeni jijini Nairobi Kenya. PICHA: Reuters
Wanafunzi wa shule ya upili ya Makongeni jijini Nairobi Kenya. PICHA: Reuters

Wadau wa elimu nchini Kenya wameshtumu agizo la serikali la ghafla la kuamrisha kufungwa kwa shule zote nchini humo baada ya wiki tatu tu shule kufunguliwa kufuatia kukamilika kwa muhula wa masomo.

Wazazi sasa wanalazimika kupanga mipango ya kusafiri kwa watoto wao badala ya kupanga kuwaondoa shuleni kwa mapumziko ya katikati ya muhula mwishoni mwa wiki kama ilivyoainishwa kwenye kalenda ya masomo iliyotolewa mapema na serikali.

Licha ya shule nyingi nchini Kenya kutumika mara kwa mara kama vituo vya kupigia kura na kujumlisha matokeo ya kura hiyo, hatua ya ghafla ya serikali ya Kenya Jumatatu kuamuru kufungwa kwa shule hizo wakati tarehe ya uchaguzi ilikuwa inafahamika kwa wizara ya elimu, inatajwa na wadau wa elimu kama ya kushtukiza na isiyofaa.

Serikali ya Kenya imekuwa ikiendesha kalenda ya masomo iliyofanyiwa ukarabati kufuatia janga la virusi vya Corona vilivyosababisha shule na vituo vingine vya masomo kufungwa kwa mihula miwili mnamo mwaka wa 2020.

Mzigo kwa wazazi

Wazazi ambao wanajipata kwenye njiapanda, kwa sasa wanalazimika kuweka mipango ya kusafiri kwa watoto wao kutoka kwenye shule za malazi badala ya kupanga kuwaondoa shuleni kwa mapumziko ya katikati ya muhula mwishoni mwa wiki hii kama ilivyoainishwa kwenye kalenda hiyo iliyokarabatiwa ya masomo iliyotolewa mapema na wizara ya elimu. Na kujipanga huko pia kunajumuisha kuwawezesha watoto wao kurejea shuleni Alhamisi wiki ijayo siku mbili baada ya kukamilika kwa zoezi la upigaji kura. Haya yakitajwa kuwa ni mapumziko ya pili madogo kwa wanafunzi wote nchini Kenya.

Na japo serikali ya Kenya inasema kuwa tangazo lake la ghafla ni la kuiwezesha tume ya uchaguzi IEBC kuwa na muda zaidi wa kujiandaa kwa uchaguzi wa Jumanne wiki ijayo, wadau wanaeleza kuwa hapakuwapo na maelezo ya kina kabla ya tangazo hilo.

Shule zilikuwa katika maandalizi ya mitihani

Shule nyingi zimekuwa zikitekeleza majaribio ya tathmini ya katikati ya muhula ambayo inatathmini wanafunzi wiki tatu baada ya kukamilika kwa mapumziko ya muhula uliopita.

Awali, waziri wa elimu Professa George Magoha alikuwa ameonesha mafadhaiko yake kuwa huenda kalenda ya masomo ikavurugwa tena kutokana na uchaguzi mkuu.

Chini ya kalenda ya masomo iliyokarabatiwa, muhula wa pili una wiki 10 za kujifunza na ulinuiwa kuhitimika Septemba 16 lakini iwapo uchaguzi wa Kenya utakumbwa na utata au hitilafu, huenda shule zikalazimika kufungwa zaidi. Lakini wadau wa elimu kama mwenyekiti wa chama cha wazazi Kenya Nicholas Maiyo wanasema kwamba patahitajika kuwapo ushauri wa kina kuwezesha urejeleaji wa masomo kwa njia salama.

Kalenda ya elimu

Muhula wa tatu na wa mwisho katika kalenda hiyo ya masomo, umepangwa kuanza Septemba 26 hadi Novemba 25, kisha mitihani ya kitaifa itafanyika.

Wadau vile vile wanaeleza kuwa mkakati wa ufunzaji utaathirika zaidi na walimu huenda wasipate nafasi ya kuwatayarisha wanafunzi ipasavyo.

Jumatatu, mwenyekiti wa tume ya uchaguzi na mipaka nchini Kenya, Wafula Chebukati katika mahojiano ya kipekee na VOA, amesema kuwa tume hiyo ipo tayari kuandaa uchaguzi mkuu na inaamini kuwa utakuwa wa haki, uwazi, unaoaminika na unaoweza kuthibitishwa na kuwataka raia wa Kenya kuwa na imani na tume hiyo.

Ni siku sita tu pekee zimebakia kwa Kenya kufanya uchaguzi wake mkuu, wa saba baada ya miaka 30 chini ya mfumo wa vyama vingi, na wa 12 baada ya kujinyakulia uhuru miaka 59 iliyopita.

Ripoti hii imeandaliwa na Kennedy Wandera, VOA, Nairobi

XS
SM
MD
LG