Wanajeshi wa ushirika unaoongozwa na Saudi Arabia nchini Yemen wamewauwa zaidi ya wapiganaji 800 wa al-Qaidah katika shambulizi kwenye mji mmoja wa kusini-mashariki unaoshikiliwa na kundi la wanamgambo kwa kipindi cha mwaka mzima, kwa mujibu wa kikosi cha ushirika.
Idadi ya vifo iliyodaiwa na ushirika haikuweza kuthibitishwa. Shirika rasmi la habari la Saudi Arabia limesema leo Jumatatu kwamba wapiganaji wa Yemen wanaoungwa mkono na vikosi vya anga vya ushirika wa kiarabu vilishambulia ngome ya al-Qaidah katika mji wa bandari wa Mukalla.
Vyanzo vya kijeshi vililiambia shirika la habari la Ufaransa, kwamba wanajeshi wa ushirika waliingia Mukalla na hawakukutana na upinzani wowote kutoka kwa wanamgambo wa al-Qaidah ambao waliondoka magharibi. Chanzo pia kilisema kituo cha mafuta kilitekwa tena wakati wa mapigano.