Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Julai 20, 2024 Local time: 11:50

Shambulizi la kushtukiza lafanyika Dallas


Polisi wa Dallas wakiwa katika eneo la tukio siku ya Alhamis.
Polisi wa Dallas wakiwa katika eneo la tukio siku ya Alhamis.

Polisi wa Dallas walisema washukiwa watatu wapo kizuizini na mshukiwa wa nne amefariki saa kadhaa baada ya mlenga shabaha kuwauwa maafisa polisi watano wakati wa shambulizi moja lililofanyika wakati wa maandamano ya amani. Maafisa polisi saba na raia wawili walijeruhiwa katika shambulizi hilo la kushtukiza, alisema Meya wa mji wa Dallas siku ya Ijumaa.

Shambulizi lilitokea Alhamis usiku wakati wa maandamano dhidi ya mauaji ya wanaume wawili weusi yaliyofanywa na maafisa polisi wazungu katika jimbo la Minnesota na Louisiana.

Sehemu kadhaa za mji wa Dallas zimeendelea kuwekwa utepe wa njano wa polisi wakati maafisa polisi wanafanya uchunguzi wa ufyatuaji risasi ambao umeonekana kuwa shambulizi baya lililosababisha mauaji kwa idara ya polisi tangu mashambulizi ya ugaidi ya Septemba 11 mwaka 2001.

Rais Obama alielezea ufyatuaji risasi uliotokea Dallas.
Rais Obama alielezea ufyatuaji risasi uliotokea Dallas.

Rais Obama aliita ufyatuaji risasi huo ni shambulizi la ukatili, kitendo kilichofanywa kwa mpangilio na chenye chuki kwa maafisa ambao walikuwa wakifanya kazi yao. Akizungumza kutoka Warsaw, Poland mahala ambapo anahudhuria mkutano wa NATO, Obama alisema polisi wana kazi ngumu sana na ufyatuaji risasi wenye kuhuzunisha unakumbusha hatari wanazokabiliana nazo polisi.

Mkuu wa polisi wa Dallas, David Brown alisema washukiwa hawakupewa ishara yeyote kwanini shambulizi liliwalenga maafisa. Brown alisema mmoja wa washukiwa aliyekamatwa ni mwanamke. Washukiwa wawili wengine waliohojiwa, Brown alisema walionekana na mifuko yenye vifaa vya jeshi na kuchochea maafisa wa polisi kufuatilia gari lao.

Picha za video za ufyatuaji risasi zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zilionesha watu wakikimbia milio ya risasi. Video pia ilimuonyesha mtu mmoja mwenye silaha akimfyatulia risasi ofisa mmoja wa polisi.

Eneo kubwa la kati kati ya mji limeendelea kufungwa. Mkuu wa polisi alisema hakuwa na uhakika kamili, kwamba washukiwa wote wamekamatwa.

Maafisa wanasema washambuliaji walikuwa na nia ya kufanya uharibifu mkubwa na mfuko mmoja uliokuwa ukitiliwa shaka umedhibitiwa na timu inayohusika na masuala ya bomu katika mji.

Mayor wa Dallas, Mike Rawlings akizungumza na wakazi wa eneo hilo.
Mayor wa Dallas, Mike Rawlings akizungumza na wakazi wa eneo hilo.

Meya wa Dallas, Mike Rawlings aliwaomba watu ambao wanafanya kazi kati kati ya mji mahala ambako ufyatuaji risasi ulitokea kutofika eneo hilo.

Polisi walitoa picha ya mtu mmoja mweusi mwenye silaha akiwa na mavazi ya kijeshi ambaye alihudhuria maandamano kama ndiye “mtu mwenye kufikiriwa” katika ufyatuaji risasi uliotokea Alhamis. Mtu huyo baadae alijisalimisha mwenyewe kwa maafisa ambao wanasema hakuhusika katika ufyatuaji risasi huo.

Maandamano ya amani ya Alhamis jioni yalihusisha kiasi cha watu 1,100 ambao walikuwa wakiandamana kupinga mauaji katika majimbo ya Minnesota na Louisiana yaliyofanyika mwanzoni mwa wiki. Matukio yote yalichukuliwa kwenye video ambayo yalipelekea maandamano katika miji mingi ya Marekani. Wizara ya sheria ya Marekani inasema inafuatilia uchunguzi kuhusiana na mauaji hayo.

Mkuu wa polisi Dallas, David Brown.
Mkuu wa polisi Dallas, David Brown.

Mauaji ya wanaume weusi ni matukio ya karibuni katika mfululizo wa ufyatuaji risasi nchini Marekani ambao uliangaliwa kwa mapana kama mifano ya polisi kutumia nguvu kupita kiasi katika kukabiliana na walio wachache.

XS
SM
MD
LG