Muimbaji taarab maarufu nchini Tanzania, Shakila Saidi amefariki dunia Ijumaa nyumbani kwake Mbagala Charambe, jijini Dar es Salaam.
Bi Shakila ambaye alianza kuimba taarab mwaka 1961, alivuma sana katika uwanja wa taarabu mkoani Tanga ambao aliimba katika bendi ya Lucky Star na Black Star. Katika miaka 1980 alijiunga na bendi ya JKT na kujizolea umaarufu mkubwa nchini Tanzania na eneo zima la Afrika Mashariki na Kati. Alistaafu kuimba katika taarabu kwenye bendi hiyo mwaka 1990.
Atakumbukwa kwa nyimbo zake maarufu ambazo zilizokuwa na ujumbe mzito sana kama "Kitumbiri", "Mapenzi yamepungua" na " Macho yanacheka."
Bi Shakila aliolewa mwaka 1960 akiwa na umri wa miaka 11. Amejaaliwa watoto 13 na wajukuu kadhaa. Atakumbukwa kwa ucheshi wake na mara nyingi alikuwa akialikwa kutumbuiza kwenye sherehe mbali mbali za harusi hasa mjini Dar es Salaam na Tanga.
Mungu ailaza roho yake mahali pema peponi. Ameen.