Serikali ya Sudan imewaachia huru takribani wanaharakati 80 wa upinzani waliokamatwa mwezi Januari wakati maafisa wa usalama walipokua wanajaribu kukandamiza maandamano na malalamiko dhidi ya nyongeza za bei za chakula nchini humo.
Kuachiwa huru kwa wapinzani hao wakiwemo baadhi ya maafisa waandamizi wa upinzani imetokea siku tatu baada ya Marekani kueleza wasi wasi wake kutokana na kukamatwa watu hao na kueleza kwamba wengi kati yao wanashikiliwa chini ya hali mbaya ya maisha.
Wafungwa waliachiliwa huru kutoka jela ya Kobar kaskazini ya Khartoum ambako walipokelewa na familia na marafiki na pia waandishi habari walialikwa na serikali kushuhudia kuachiliwa kwao. Mshauri muandamizi wa Rais Omar al Bashir alisema rais aliamrisha kuwa watu wote waachiliwe huru.
Kijana wa Waziri Mkuu wa zamani Sadiq al Mahd, Al sidiq al Sadiq aliwambia waandishi habari kwamba bado hawajihisi kuwa na uhuru kamili kwa sababu baadhi ya wenzao bado wanashikiliwa na maafisa wa usalama.
Miongoni mwa viongozi walioachiliwa Jumapili ni Fadlalla Burma Nasir kiongozi muandamizi wa chama cha upinzani cha Umma na Sarah Nugdallah mwanaharakati mtetea haki za wanawake wa kundi la Amal Habbani.
Maandamano ya hapa na pale yamekua yakifanyika tangu Januari mwaka huu mjini Khartoum na miji mingine ya Sudan baada ya vyama vya upinzani na wanaharakati kutoa wito wa kufanyika maandamano dhidi ya serikali na kulalamika dhidi ya kupanda bei ya vyakula.
Polisi wa kupambana na ghasia na polisi nchini humo wamefanikiwa kutawanya maandamano hayo.